Dk Shein Ajivunia Upatikanaji wa Maji Safi na Salama Zanzibar

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo huduma ya maji safi na salama katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba.

Dk. Shein aliyasema hayo o kwa nyakati tofauti katika ziara yake ya Kichama katika Wilaya ya Kusini Unguja.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imefanya juhudi kubwa za kutafuta fedha kwa njia ya mkopo zaid ya bilioni 64.4 kutoka Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kwa ajili ya kuimarisha sekta ya maji pamoja na kiasi cha Tsh. Bilioni 36 kwa ajili ya miundombinu ya maji.

Jitihada zinafanywa katika kuhakikisha tatizo la maji linamalizika katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar likiwemo Jimbo la Makunduchi.

Katika ziara hiyo, Dk. Shein aliweka jiwe la msingi mradi wa Chama wa maduka na kupata maelezo pamoja na kukagua ujenzi wa ukumbi mpya wa mikutano uliopo katika eneo la afisi ya CCM Wilaya ya Kusini Unguja.

Dk. Shein pia, aliweka jiwe la msingi katika jengo la ushirka wa UWT, Daima Tupendane. Aidha, alifika Tawi la CCM Mzuri kuangalia ukarabati wa afisi ya Tawi la CCM na kusalimiana na wanachama wa CCM wa Wadi ya Mzuri na kutoa kadi za CCM kwa wanachama wapya 203.

Mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika jingo la ushirika wa UWT, Daima Tupendane, Dk Shein alipongeza juhudi za ushirika huo na kuahidi kuwasaidia walipofikia katika ujenzi huo pamoja na kuwapa mtaji wa kuanzisha bekari ya mikate. Dk. Shein alieleza juu ya suala zima la ajira kwa vijana na jinsi serikali ilivyojipanga juu ya hilo.

Baada ya hapo Dk. Shein alikagua ukarabati wa Tawi la CCM Bwejuuambapo alipokelewa kwa shangwe kubwa na kuwapa kai wanachama wapya 186 wakiwemo vijana na baadae aliwasilimia.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali alisema kuwa ziara zake zimewaonesha njia wanaCCM katika msimamo wa kuimarisha Muungano na vipi unatakiwa ulindwe na udumishwe sanjari na Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.

Akiwa katika majumuisho ya Mkoa huo baada ya kumaliza ziara yake, Dk. Shein alisema kuwa uhai wa chama umo katika vikao, na kusifu juhudi zilizofanywa na viongozi wa chama pamoja na juhudi za utekelezaji wa Ilani na Sera za CCM na kuupongeza Mkoa huo kwa kingiza wanachama wapya.

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliupongeza Mkoa huo wa Kusini kwa kuendelea kuenzi na kuitunza historia ya ASP hadi kufikia CCM nakueleza kuwa ziara hiyo imefana sana.

Aidha, alieleza kuwa Mapinduzi ya Januari 1964, ndio mkombozi wa nchi na lazima wafundishwe vijana jinsi Zanzibar ilivyokombolewa na kwa nini Mapinduzi yametokea. Aidha, alieleza umuhimu wa Muungano na mafanikio yake yaliopatikana na kusisitiza utadumishwa daima.

Viongozi wa CCM ni lazima wajue kuwa wanajukumu la kuwatumikia wanaCCM il kuweza kuimarisha chama.

Alisema Mkoa wa Kusini kujitahidi kuimarisha chama na kuhakikisha ofisi za Matawi zinakuwa na nyenzo za kufanyia kazi huku akieleza jinsi alivyofurahishwa na mashirikiano yaliopo kati ya Wabunge na Wawakilishi na kusisitiza kuzidisha mashirikiano hayo.

Alieleza kuwa anafarajika sana kuwaona viongozi wa Majimbo wanakuwa kitu kimoja na kueleza matumaini yake katika ziara hiyo kwani wameanza vizuri na CCM ina kasi kubwa.

Uongozi wa Mkoa huo aliwataka kujiandaa katika uchaguzi ujao wa mwaka 2015 na kuhakikisha CCM,inashinda uchaguzi huo.