Mama Tunu Pinda Awataka Watanzania Kuchangia Kazi za Mungu

Tunu Pinda akiwa anaonesha DVD yenye jina la Mungu Wetu Halinganishwi iliyo imbwa na kwaya ya Kanisa la TAG Mwenge wanaoshuhudia ni kulia kwa Mama Pinda ni Mchungaji kiongozi Abdiel Mhini kulia mwenye kilemba ni Mchungaji Grace Mainoya anayefuatia ni Askofu wa jimbo la Mashariki Kaskazini  Spear Mwaipopo Mama Tunu Pinda alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa DVD hiyo.


 
MKE WA WAZIRI MKUU Mama Tunu Pinda amewataka Watanzania wajenge tabia ya kuchagia kazi za Mungu ili kuwasaidia watu wengine wapate fursa ya kulisikia neno la Mungu bila vikwazo. Ametoa wito huo Aprili 28, 2013 wakati wa ibada ya uzinduzi wa albamu ya “Mungu Wetu Halinganishwi” iliyofanyika kwenye Kanisa la TAG, Mwenge jijini Dar es Salaam.
 
“Mungu Wetu Halinganishwi” ni albamu za DVD, VCD na CD zilizotolewa na kwaya ya Imani ambayo ni kwaya kuu ya kanisa hilo. Albamu hiyo ina nyimbo nane. Zaidi ya sh. milioni 12 zilipatikana ikiwa ni ahadi na fedha taslimu kutokana na mnada wa DVD za albamu hiyo.
 
“Naomba kutoa changamoto kwa kila mmoja wetu aliyefika mahali hapa mchana huu, tujiulize ni kwa kiasi gani tumesaidia kupeleka Neno la Mungu kwa watu wenye uhitaji wa kulisikia Neno na hawana uwezo wa kulisikia Neno hilo? Ni kwa kiasi gani tumeshiriki kuchangia huduma ya Uinjilisti ili wenye kiu ya Neno waweze kuamini na hatimaye kuokoka?”, alisema.
 
Mama Pinda alisema Biblia Takatifu inawakumbusha wanadamu wote kwamba kuamini, kubatizwa na hatimaye kuokoka si hiari ya mwanadamu bali ni amri ya Mwenyezi Mungu, na akasisitiza kuwa ni wajibu wa kila mmoja kuwasaidia watu wenye kiu ya neno la Mungu ili kuhakikisha wanapokea neno la Mungu.
 
“Tujiulize ni jinsi gani tutawasaidia wapate kulisikia na kuliamini Neno la Mungu na hatimaye kuokoka. Tukumbuke kwamba hawa ndiyo majirani zetu ambao Biblia inatukumbusha kuwapenda kama tunavyojipenda sisi wenyewe,” alisisitiza.

DVD yenye jina la Mungu Wetu Halinganishwi

 
Alisema umefika wakati wa Watanzania kuanza kuchangia huduma za kusambaza neno la Mungu iwe kwa nyimbo kama walivyofanya Imani Choir au kwa njia nyingine kwani watu wako radhi kuchangia harusi kuliko kuchangia kazi ya Mungu.
 
“Sisi sote tu mashahidi wa jinsi ambavyo tumekuwa mstari wa mbele katika kuchangia harusi lakini tukilegelega kuchangia kazi ya uenezaji injili. Nasi tunaweza kuwaunga mkono Kwaya ya Imani kwenye kazi hii kwa kutumia mali zetu. Naomba nitumie fursa hii kuwasihi sana wote mliopo hapa tujitoe kwa mali zetu ili tuwawezeshe Imani Choir kuifanya kazi hii kwa ukamilifu,” alisisitiza.
 
Mapema, akitoa mahubiri ya ibada hiyo ya kuweka wakfu ya kuzindua albamu ya “Mungu Wetu Halinganishwi”, Makamu wa Askofu wa Jimbo la Mashariki Kaskazini, Mch. Spear Mwaipopo, alisema mtu akifanya kazi ya Mungu kamwe haiendi bure ili mradi atambue kuwa anaifanya kazi ya Mungu. Aliwasihi waumini na wageni waliohudhuria uzinduzi huo kutambua ukuu na mamlaka ya jina la Yesu.
 
Katika risala iliyosomwa na Katibu wa kwaya ya Imani, Bi. Janet Masaga, ilielezwa kwamba  jumla ya sh. milioni 25/- zinahitajika kwa ajili ya kununua basi aina ya Coaster kwa ajili ya kuwasaidia kubeba wanakwaya hao wenye nia ya kupeleka injili vijijini.
 
Naye Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo, Mch. Abdiel Meshack Mhini aliongoza maombi kwa ajili ya Taifa la Tanzania ambapo alitumia fursa hiyo pia kuwaombea viongozi wa Kitaifa, kuliombea Bunge la Tanzania na vikao vilivyosalia mbele yake. Alimshukuru Mama Tunu Pinda kwa kutenga muda wake na kukubali kuizundia albamu ya kwaya kuu ya kanisa hilo.