Bunge la EAC Lapitisha Sheria ya Kituo Kimoja cha Forodha

Spika wa Bunge la Afrika ya Mashariki, Magreti Nzziwa Nantongo (Kulia) akiwa kwenye moja ya majukumu.

Na James Gashumba, EANA

BUNGE la Afrika Mashariki (EALA) Alhamisi lilipitisha sheria ya kuanzishwa kwa Kituo Kimoja cha Forodha Mipakani (OSBP) katika nchi tano wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Azimio hilo liliibuliwa na Baraza la Mawaziri la EAC ni moja ya agenda za kukuza mwingiliano wa watu na biashara katika jumuiya hiyo. Nchi wanachama wa jumuiya hiyo ni pamoja na Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi.

Sheria hiyo itaweza kutumika katika uendeshaji wa vituo vya forodha vya mipakani, uratibu na usimamizi wake. Hata hivyo sheria hiyo haitaathiri haki ya nchi mwanachama ya kufanya uchunguzi kwa minajili ya ulinzi, usalama, usalama wa umma na utii wa
sheria.

Sheria hiyo pia imeorodhesha vituo vilivyo katika utaratibu huo wa OSBP. Vituo hivyo vya mipakani ni pamoja na Taveta – Holili na Namanga (Kenya-Tanzania), Busia na Malaba (Kenya –Uganda) na Kanyaru – Akanyaru(Burundi-Rwanda). Vingine ni Mutukula (Tanzania-Uganda), Gasenyi – Nemba (Burundi-Rwanda) na Lungalunga-Horohoro (Kenya-Tanzania).

Mjadala juu ya sheria hii ulitanguliwa na uwasilishwaji wa ripoti ya Kamati ya Mawasiliano, Biashara na Uwekezaji (CTI) iliyowasilishwa na Mwenyekiti wake, Dan Kadega kutoka Uganda.

Sheria hiyo inataka nchi wanachama kuendeleza, kuboresha, kuweka miundombinu ya kisasa na kuimarisha teknolojia ili kuhakikisha kuwepo kwa ufanisi katika utekelezaji wa sheria hii. Iliwasilishwa baada ya mjadala ulifanyika katika nchi wanachama Machi
na Aprili, mwaka huu ili kupata maoni kutoka kwa wadau wakiwemo maofisa wa forodha, mawakala wa mizigo na jamii ya wafanyabiashara.

Utaratibu wa OSBP umekuwa ukitumika katika baadhi ya vituo vya forodha vya mipakani kwa makubaliano baina ya nchi na nchi lakini ilibainika kwamba sheria juu ya utaratibu muafaka utakaotumika katika nchi zote wanachama unahitajika, kwa mujibu wa ripoti ya kamati.