‘Watakiwa Kutumia Rasilimali Kupambana na Ukimwi’

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi

Na Magreth Kinabo, Maelezo

JAMII imeshauriwa kuwekeza rasilimali kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi wakati akitoa tamko kuhusu maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ambayo hufanyika Mei 25, kila mwaka.

Dk. Mwinyi alisema moja wapo ya changamoto katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo ni tuna tishio la upatikanaji wa rasilimali kwa ajili ya kuendeleza hatua zilizofikia kuutokomeza ugonjwa huo. Mfano misaada iliyokuwa ikitolewa kwa nchi za Afrika imepungua cha dola za Marekani bilioni 3.6 kwa mwaka, hivyo Tanzania ni miongoni mwa nchi hizo.

“Kwa hali hiyo hatuna budi kila mmoja katika nafasi aliyonayo kuwekeza kwa ajili ya mapambano dhidi ya malaria na hatimaye kutokomeza malaria katika nchi yetu ya Tanzania kama kauli mbiu inavyosema;,” alisema Dk. Mwinyi huku akisitiza umuhimu wa kuwekeza na ushirikiano kati ya jamii na wadau mbalimbali.

Aliitaja kauli mbiu hiyo kuwa ni ‘Wekeza kwa Maisha ya Baadae; Tokomeza malaria”.
Alisema serikali inajipanga ili kuhakikisha inatenga fedha nyingi za ndani za kupambana na ugonjwa huo. Aliitaka jamii kuwahi matibabu mara dalili za ugonjwa huo, zinapojitokeza kwa kuwa unatibika kwa kuwahi matibabu, pia kwa kufanya hivyo inawezekana kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.

Huku akiwataka wananchi kuendelea kulala kwenye chandarua chenye dawa kila siku na kutumia mikakati iliyowekwa ili kuweza kupambana na ugonjwa huo. Alisema changamoto nyingine ni  imani potofu nayo ni kikwazo  katika safari ya kutokomeza ugonjwa huo.Hivyo  jukumu la serikali ni kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuwa na uelewa.

“Haiwezekani dawa inayotumika kuua mazalia ya mbu ikaeneza wadudu wengine,” hata hivyo alisema dawa hiyo haiuwi wadudu wote.

Dk. Mwinyi alisema dawa sahihi ya kutibu ugonjwa huo ni dawa ya Mseto. Akizungumzia kuhusu tafiti mbalimbali zinafofanywa juu ya kupambana na ugonjwa huo zinawekwa kabatini, Dk. Mwinyi alisema si sahihi kwani sera nyingi zinategemea ushahidi wa tafiti.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria, Renata Mandike alisema mikoa inayoongoza kuwa na ugonjwa huo ni Kigoma, Katavi, Geita, Lindi na Mara.