Sethi Kamuhanda Ahimiza Uadilifu, bidii Kwa Watumishi wa Umma

Baadhi wa waajiriwa wapya kutoka wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wakimsikiliza katibu Mkuu wa wizara hiyo Sethi Kamuhanda (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi yaliyofanyika leo katika ukumbi wa mikutano uliopo uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Barnabas Ndunguru akitoa maelezo kuhusu mafunzo elekezi kwa watumishi wapya walioajiriwa na wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/13 leo katika ukumbi wa mikutano uliopo uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango Gasper Mwembezi

Na Anna Nkinda – Maelezo

WATUMISHI wa Umma wametakiwa kufanya kazi zao kwa uadilifu, bidii na kujituma huku wakifuata maadili ya kazi zao kwa kufanya hivyo wataweza kutekeleza malengo ya Serikali ya kuwahudumia wananchi kama wanavyotarajia kupata huduma nzuri.

Wito huo umetolewa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Sethi Kamuhanda wakati akifungua mafunzo elekezi ya siku mbili kwa wafanyakazi wapya yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kamuhanda alisema kuwa uvumilivu unatakiwa mahali popote pa kazi na lazima watumishi hao wawe na uwezo wa kukabiliana na changamoto watakazokutana nazo kwa kufanya kazi kwa bidii na kujituma na siyo kukata tamaa kwani mtu akifanya kazi kwa bidii viongozi wake wataiona kazi anayoifanya na kumuhitaji mara kwa mara.

Waajiriwa wapya kutoka wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, wakurugenzi wa Idara na Baadhi ya wafanyakazi wa wizara hiyo wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa ufunguzi wa mafunzo elekezi leo uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam. Watatu kushoto mstari wa mbele ni katibu Mkuu wa wizara hiyo Sethi Kamuhanda.

Aidha Kamuhanda alisema kuwa mtumishi wa sekta ya umma anafanya kazi ya kuwatumikia wananchi bila ya kubagua wala kupendelea hivyo basi hapaswi kuchagua kituo cha kufanyia kazi kwakuwa hata wananchi walioko nje ya miji wanatakiwa kupata huduma sawa na wananchi wa mijini.

“Msiwe na tabia ya kuchagua maeneo ya kufanyia kazi kwani mtumishi wa umma anapangiwa kazi na mwajiri wake katika kituo chochote kile na huko mikoani ambako watumishi wengi hawapendi kwenda ndiko ambako utajifunza mambo mengi zaidi na kuweza kukabiliana na changamoto za kazi”, alisema Kamuhanda.

Katibu Mkuu huyo pia aliwasihi wafanyakazi hao kuwa na tabia ya kujifunza kutoka kwa watumishi waliowakuta kazini wenye uzoefu wa kazi na kutojifanya wajuaji kwani kwa kufanya hivyo watajiongezea  ujuzi wa kazi na kufika mbali zaidi. Akitoa maelekezo kuhusiana na mafunzo hayo Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Barnabas Ndunguru alisema kuwa waajiriwa wapya wanatakiwa kujua sheria, kanuni na taratibu zinazoendesha utumishi wa umma.

Ndunguru alisema, “Mafunzo elekezi kwa watumishi wapya Serikalini yanawawezesha kupata ufahamu wa mambo mbalimbali kupitia mada zitakazofundishwa ambazo baadhi yake ni majukumu ya wizara, maadili katika mtumishi wa umma, wajibu wa kupiga vita rushwa mahali pa kazi na huduma kwa mteja”.

Alimalizia kwa kusema kuwa mafunzo elekezi  yatawawezesha watumishi hao kujitambua kuwa wao ni watumishi wa umma na kwamba wanatakiwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na yataimarisha mahusiano kiutendaji kati ya watumishi wapya, wakuu wa Idara na vitengo vyote na watumishi wote wa wizara. Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2012/13 imeweza kuajiri watumishi wapya 30 ambao wengi wao ni vijana kutoka kada mbalimbali.