Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
MAKAMO Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza kuimarishwa kwa amani, umoja na mshikamano na kueleza kuwa vurugu sio utamaduni wa wananchi wa Zanzibar.
Dk. Shein aliyasema hayo leo kwa nyakati tofauti katika ziara yake ya Chama katika Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Chama Mjini. Makamo Mwenyekiti huyo alieleza kuwa amani na utulivu ndio msingi wa mafanikio na ndio maana chama hicho cha CCM kimekuwa kikisimamia na kudumisha jambo hilo kwa kutambua umuhimu wake.
Alisisitiza kuwa tayari Zanzibar imeshajijengea sifa kubwa Kimataifa kutokana na mafanikio makubwa yaliopatikana katika kuimarisha na kuiendeleza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa, hivyo kujitokeza kwa watu wachache kutaka kuvuruga amani serikali haitowafumbia macho.
Alieleza kuwa wananchi wote wa Zanzibar wana haki sawa na ndio maana Serikali anayoiongoza chini ya chama cha Mapinduzi haimbagui mtu kwa jinsia, rangi, dini ama ukabila. Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliyo na mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa haitomvumilia mtu yeyote atakaevuruga amani na utulivu uliopo nchini.
Katika hotuba zake, Dk. Shein aliwasisitiza wanaCCM kuendeleza utamaduni wao wa kuimarisha amani na utulivu na kuzidisha mashirikiano kwani ndio ngao ya ushindi wa chama hicho.
Aidha, Dk. Shein alisisitiza kuwa Serikali anayoiongoza itaendelea kuyalinda na kuyadumisha Mapinduzi ya Januari 12, 1964 sanjari na kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mapema Dk. Shein alipokea taarifa ya kazi za Chama ya Mkoa wa Mjini na baada ya hapo alifika Kisiwandui na kwa ajili ya kuzindua rasmi Benki ya SACCOS ya Umoja wa Wajasiriamali wadogowadogo na kueleza kuwa hatua hiyo ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Baada ya hapo Makamu huyo wa CCM Zanzibar alikwenda Vikokotoni kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi jengo jipya la ghorofa mbili la Tawi la CCM Vikokotoni lililojengwa kwa ubia kati ya Tawi na mfanyabiashara.
Dk. Shein alimalizia ziara yake kwa Wilaya ya Mjini, Dk. Shein alitembelea maskani ya Kisonge iliyopo Michenzani na kuangalia uharibifu uliotokea baada ya kuchomwa moto kwa maskani hiyo wakati wa vurugu zilizotokezea hivi karibuni na kusababisha hasara kubwa ya zaidi ya milioni 50.
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwakabidhi kadi wanachama wapya 270 kutoka Jumuiya zote za CCM zikiwemo wazazi, Umoja wa Wanawake na UVCCM na baadae alisalimiana na wana CCM na kuwataka wanaCCM kuwafundisha siasa vyama vyengine ambavyo vimeonesha kutoelewa maana na umuhimu wa amani na utulivu.
Katika ziara hiyo burudani mbalimbali zilitumbuiza zikiwemo ngoma, nyimbo, mashairi, tenzi pamoja na burudani maalum iliyotolewa na vijana wa CCM kutoka Ilala, Dar-es-Salaam waliyoitoa katika viwanja vya Kisonge mjini Zanzibar. Ziara hiyo itaendelea kesho katika Wilaya ya Amani.