Dawa za Kuongeza Akili Zaingia Nchini

Duka la madawa


MTINDO wa maisha, ulaji na msongo wa mawazo, vimewasababishia Watanzani wengi maradhi lukuki hata vifo.

Hata hivyo, wataalamu wa afya kutoka Afrika Kusini wamekuja na dawa maalumu, zilizo na uwezo wa kurudisha kumbukumbu, kuongeza upeo darasani, kuondoa sumu mwilini na kumfanya mzee kuonekana kijana. Dawa hizo zinazotumia vitamini zilizomo kwenye vyakula vya kila siku, zina uwezo wa kuongeza kiwango cha uelewa kwa mwanafunzi au mfanyakazi.

Kiwango hicho cha uelewa kitaalamu unatambulika kama ‘IQ’. Mratibu wa dawa hizo hapa nchini, John Haule anasema kuwa dawa hizo zina uwezo wa kufanya kazi kwa haraka.

“Virutubisho hivi ni vizuri kwa wale wanaokwenda katika mitihani au wanataka kufanya kazi inayohitaji umakini wa hali ya juu,” anasema Haule na kuongeza: “Zimetengenezwa kwa vyakula tunavyotumia na siyo kemikali.”

Haule ambaye ni mtaalamu wa tiba asili na mimea anasema kwamba mtindo wa maisha na vyakula vinavyoliwa na watu mara kwa mara kwa sasa huufanya mwili kuhifadhi sumu nyingi mwilini. Anasema kuwa dawa hizo pia zina uwezo kuondoa sumu mwilini na kuufanya mwili wa binadamu kurejesha rangi yake halisi na kumeng’enya vizuri chakula anachokula.

Haule anayefanya kazi pamoja na Shirika la Nativa linalotengeneza dawa hizo la nchini Afrika Kusini, anaeleza kuwa tangu kuingiza dawa hizo nchini watu wengi wamejitokeza kuzihitaji. Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Gaudensia Simwanza anasema kuwa mamlaka hiyo inazitambua dawa hizo kama virutubisho vya chakula, zimesajiliwa na ni salama kwa binadamu.

“Tuna taarifa kuwa bidhaa za ‘Go Woman’ na ‘Go Man’ zimesajiliwa na ni salama,” anasema.

Dawa nyingine zinazotengenezwa na kampuni hiyo zimetajwa kuwa na uwezo wa kuunda mifupa kwa watu wazima na majeraha ya wagonjwa wa kisukari.
CHANZO: Gazeti Mwananchi