RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amezitaka Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama kudhibiti wimbi la wizi wa mazao na
mifugo lililoshika kasi Zanzibar hivi sasa.
Dk. Shein amesema suala hilo lazima lishughuklikiwe vizuri na kwa umakini mkubwa kwa sababu hatua iliyofikiwa sasa na vitendo vya baadhi ya wezi kukata sehemu za viungo vya mifugo kama ng’ombe na kuwaacha wazima sio tu kuwa ni ukatili lakini ni vitendo ambavyo haviwezi kufikiriwa kufanywa Zanzibar.
Rais ametoa wito huo wakati akihitimisha majadiliano ya Mkutano wa Tathmini ya Taarifa ya Utekelezaji Mpangokazi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Idara ya Uratibu Mamlaka za Mikoa na
Serikali za Mitaa uliofanyika jana Ikulu.
“Ni vitendo vibaya na vya kikatili kukata baadhi ya viungo vya mnyama bila kuchinjwa huku ukimwacha akihangaika kwa maumivu. Lazima tuwe makini na hatua za kuchukua kwa kuwa wanaofanya vitendo hivi si watu wa kawaida” alisema Rais na kueleza hofu yake kuwa nyama hiyo huishia kuuzwa kwa matumizi mbalimbali ya wananchi kitendo ambacho kinaingilia hata imani ya dini.
Sambamba na agizo hilo Dk. Shein amewakumbusha viongozi na watendaji wa mamlaka hizo kuelewa kuwa mamlaka hizo ndizo zilizo karibu na jamii na ndizo zinazoshughulikia masuala ya wananchi hivyo kila wakati wawe
tayari kupokea na kutafuta njia za kukabiliana na changamoto mbalimbali kutoka kwa wananchi hao.
“Huko mliko ndiko kwenye wananchi…sisi wote humu (kikaoni) tunaishi katika maeneo ya mamlaka zenu hivyo hoja zitakuja, malalamiko yatakuja na hata pongezi wakati mwingine wananchi watakujanazo zote tuzipokee”
Dk. Shein alisisitiza.
Aliwasisitizia washiriki wa mkutano huo wakiwemo wakuu wa Mikoa na Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya pamoja na Watendaji wa Manispaa, Mabaraza ya Miji na Halmashauri kuwa ni wajibu wao kujibu hoja za wananchi kwa kadri wanavyozielewa na kwa kufuata Sheria na taratibu zinazowaongoza.
Rais alieleza kuridhishwa kwake na mwelekeo mzuri wa ukusanyaji mapato katika Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa na kuzitaka ziongeze jitihada zaidi ili zifikie hatua nzuri ya kupunguza utegemezi wa
ruzuku na hatimae ziweze kujitegemea.
“Tuongeze kasi ya utekelezaji majukumu yetu kwa kuongeza kasi ya ushirikiano, kasi ya mashauriano na kupunguza kasi ya kulaumiana na tukubali tujisahihisha pale tunapokosolewa”aliwasisitizia viongozi na
watendaji mamlaka hizo.
Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharriff Hamad ametoa wito kwa watendaji wa Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha wanakuwa makini katika matumizi ya fedha za makusanyo katika mamlaka zao.
Akichangia katika mjadala huo Maalim Seif amesema mwelekeo mzuri wa makusanyo ya fedha katika mamlaka hizo ni ishara ya mwitikio mzuri wa wananchi kulipa kodi mbalimbali hivyo matokeo mazuri ya matumizi ya
fedha hizo katika utoaji huduma yatakuwa kichocheo zaidi kwao kuendelea kulipa kodi kama itakiwavyo.
“Nimetiwa moyo na hatua ya ukusanyaji mapato katika Manispaa, Mabaraza ya Miji na Halmashauri hivyo lazima watendaji wawe makini katika matumizi ya fedha hizo kwani mapato yanapokuwa mazuri wananchi
wanatarajia huduma nzuri kutokana ma matumizi ya fedha zao,” alieleza Maalim Seif.
Makamu wa Kwanza wa Rais alizungumzia pia kuhusu vitendo vya wizi wa mazao vinavyoendelea hivi sasa Unguja na Pemba na kueleza kuwa vitendo hivyo vikiendelea vinavyoweza kuwavunja moyo wakulima hivyo alizitaka Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa ziongeze jitihada za kukabiliana nazo.