BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limesitisha shughuli zake ghafla mjini Dodoma baada ya kutokea mvutano kati ya wabunge kadhaa wa upinzani (CHADEMA) na Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai usiku huu.
Hali hiyo imetokea wakati Mbenge wa CCM Jimbo la Iramba, Mwigulu Nchemba na kutoa tuhuma ya udini kwa viongozi wa Chadema tuhuma ambayo ilikanushwa kwa taarifa na mmoja wa wabunge wa Chadema. Baada ya hapo Mbunge Nchemba aliendelea kuzungumza na akadai watu waliompa taarifa za kuwepo na udini Chadema wapo tayari kutoa ushaidi, ndipo Mbunge Tundu Lissu aliposimama akiomba utaratibu kwa Naibu wa Spika.
Naibu wa Spika alimkatalia Tundu Lissu kufanya hivyo kwa kuwa alikuwa amenyanyuka zaidi ya mara moja kutoa taarifa na kuhusu utaratibu. Kitendo hicho cha Lisu kunyanyuka tena kilimuudhi Naibu Spika hivyo kuamuru atolewe nje ya Bunge huku bunge likiendelea. Huku kitendo hicho kikiendelea baada ya wabunge wa upinzani walisikika wakisema “hatoki mtu nje, huu ni uonevu” kelele na zogo bungeni zilitawala kidogo ndipo askari wa bunge walifanikiwa kumshawishi Lissu na kumtoa nje huku wabunge wengine kadhaa wa Chadema yaani Ezekiel Wenje, Godbless Lemma, Joseph Mbilinyi (Mr. II) na Peter Msingwa wakibaki wamesimama wakioneshwa kutoridhika na amri ya Naibu Spika.
Naibu Spika aliamuru nao watolewe nje ndipo walipogoma kutoka hivyo bunge kusitishwa hadi kesho. Kituo cha Televisheni ya Taifa cha TBC 1 kililazimika kukatisha matangazo yake ghafla kutokana na mvutano uliokuwa unaendelea bungeni.
Zaidi endelea kufuatilia mtandao huu utakujuza nini kilichoendelea baada ya Bunge kusitishwa.