WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara (Mb) ameunda Kamati ya kufanikisha Ushindi ya Timu ya Mpira wa Miguu ya Tanzania (Taifa Stars), ikiwa ni jitihada za Serikali kuhakikisha Taifa Stars inawezeshwa na kuandaliwa ipasavyo ili kufanya vizuri katika michuano inayoikabili timu hiyo.
Timu ya Taifa ya mpira wa Miguu kwa Wanaume (Taifa Stars) kwa sasa ipo kwenye michuano ya kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Brazil mwaka 2014. Katika Afrika, Tanzania (Taifa Stars) imepangwa kundi ‘C’ kati ya makundi 10, kundi linalojumuisha timu za Ivory Coast, Morocco, Gambia na Tanzania yenyewe.
Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana, Dk. Mukangara alisema kwa sasa Taifa Stars ipo katika nafasi nzuri ya kufuzu, kwani inatakiwa ishinde mechi zote tatu (3) na kuongoza kundi C na baadae iingie katika Timu kumi (10) bora na kisha zipatikane Timu tano (5) kutoka Afrika, ambazo zitakuwa zimefuzu kwenda Brazil katika Fainali za Kombe la Dunia kwa mwaka 2014.
Aliwataja wajumbe 11 watakaounda kamati hiyo na maeneo wanayotoka/nafasi zao kwenye mabano ni pamoja na Mohamed Dewji (Mbunge) ambaye atakuwa kiongozi wa wajumbe, Teddy Mapunda (Montage), Dk. Ramadhani Dau (Mkurugenzi Mtendaji NSSF), Dioniz Malinzi (Mwenyekiti BMT), Abji Shabir (New Africa Hotel), George Kavishe (TBL), Mohamed Raza (Zanzibar), Leodger Tenga (Rais wa TFF), Joseph Kusaga (Clouds), John Komba (Mbunge), Zitto Kabwe (Mbunge).
“Sasa kwa kuzingatia uzito wa jukumu lililo mbele yetu na kwa Taifa Stars kwa ujumla; Serikali imeunda Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars…Jukumu la msingi la Kamati hii ni kuhakikisha Taifa Stars inawezeshwa na kuandaliwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuunda kikundi cha kuishangilia timu ya Taifa ndani na nje ya nchi,” alisema Dk. Mukangara aktika taarifa yake.
Alisema kamati hiyo inatakiwa kuanza kazi mara moja na itakabidhiwa hadidu za rejea kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo zitakazowaongoza kutekeleza majukumu yao na pia inaruhusiwa kushirikisha wadau mbalimbali kadri itakavyoona inafaa.
Aliongeza kwa upande wa Serikali inaahidi kutoa ushirikiano utakaohitajika katika kuhakikisha Kamati hii inafanya kazi vizuri ili kuiwezesha Taifa Stars kushinda Mechi zote zilizombele yetu. “Kwa mara nyingine Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inapenda kuwapongeza Taifa Stars, kwa kazi nzuri ambayo wameishaifanya ikiwemo ushindi wa Bao Tatu kwa Moja dhidi ya Morocco. Watanzania wote na Wadau wa Soka nchini wamefurahishwa sana na mafanikio yaliyofikiwa na Taifa Stars na yenye kutupa matumaini katika kuitayarisha Taifa Stars kufuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia kwa mwaka 2014 nchini Brazil.”
Aidha aliwaomba Watanzania wote, kuiunga mkono Taifa Stars na Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars kwa hali na mali katika kuhakikisha timu yetu inafuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia.
“Kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri Mkuu naomba niwasilishe salaam zao za kuwapongeza Vijana wetu wa Taifa Stars, pamoja na benchi la ufundi likiongozwa na Kocha Mkuu Kim Poulsen. Kwa pamoja wanaomba Taifa Stars iendelee kujipanga kwa mechi zijazo. Nawahakikishia kuwa Serikali, Watanzania na wadau wa Soka nchini wapo nyuma yao,” alisema waziri.