Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali, Davis Mwamunyange kufuatia kifo cha Meja Jenerali mstaafu, Makame Rashid ambaye aliaga dunia Aprili 14, 2013 katika Hospitali ya Jeshi la Wananachi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo, Dar-es Salaam.
Katika salamu hizo Rais wa Zanzibar amemuelezea marehemu Makame kuwa katika enzi za utumishi wake kwa umma ikiwemo Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, alikuwa msikivu na mchapa kazi hodari wa kupigiwa mfano.
Aidha, Dk. Shein alimuelezea Meja Jenerali Makame kuwa amechangia sana kuimarisha nidhamu na maendeleo ya Jeshi la Kujenga Taifa katika nafasi yake ya Mkuu wa Jeshi hilo. Dk. Shein katika salamu hizo alieleza kuwa yeye mwenyewe binafsi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wa Zanzibar kwa jumla, wamehuzunishwa na kifo cha kiongozi huyo ambae ametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika nafasi mbali mbali za utumishi wake.
“Marehemu anatambulika kuwa alikuwa shupavu na muadilifu alieweka mbele maslahi ya nchi yetu”, alisema Dk Shein katika rambirambi zake kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania.
Dk. Shein katika salamu hizo alieleza kuwa kupitia kwa Mkuu huyo wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, kufikisha salamu za rambi rambi kwa Maafisa na Wapiganaji wote wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama kufuatia msiba huo. Aidha salamu za pole zilitumwa kwa ndugu, marafiki na familia ya marehemu Meja Jenerali Mstaafu Makame Rashid, na kuwaombea moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu.
“Mwenyezi Mungu ampe malazi mema peponi Marehemu Meja Jenerali Mstaafu Makae Rashid”, zilimalizia salamu hizo za rambirambi.
Meja Jenerali Makame alijiunga na JWTZ Oktoba mosi 1964 na kustaafu Oktoba 22, 2001 akiwa ametumikia Jeshi kwa miaka 37 na siku 22. Meja Jenerali Makame anatarajiwa kuzikwa kesho katika kijiji cha Mnyawa, Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara. Makame ameacha mjane, watoto tisa na wajukuu wanane.