WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imesema kuwa mafanikio makubwa yamepatikana ndani ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein hasa katika maendeleo ya ujasiriamali, mifugo na uvuvi Zanzibar. Uongozi wa Wizara hiyo umesema hayo katika mkutano wa kuangalia utekelezaji wa mpango kazi kwa kipindi cha Julai 2012 hadi Machi 2013.
Mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake Rais Dk. Shein pia, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad alishiriki pamoja na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.
Uongozi huo, chini ya Waziri wake, Abdilahi Jihad Hassan akitoa muktasari wa mpango kazi wa Wizara hiyo alisema kuwa mkakati mkubwa umeelekezwa katika kuwajengea uwezo wazalishaji wa mazao ya baharini na wafugaji wa mifugo. Waziri Jihad alieleza kuwa Wizara imeweza kupata msaada mkubwa kutoka kwa washirika wa maendeleo kwenye sekta hizo ambapo sekta ya uvuvi ndio imepata msaada mkubwa hasa katika suala zima la ufugaji wa samaki.
Alisema kuwa nchi kama China, Jamhuri ya Korea na Oman zimekuwa karibu sana na Wizara katika kuendeleza uvuvi na ufugaji wa mazao ya baharini ikiwa ni pamoja na kuweko makubaliano na nchi hizo ili kuendeleza uvuvi kwa manufaa ya pande zote.
Hata hivyo, uongozi huo ulieleza kuwa Wizara imelenga kuanzisha vituo vya mifugo na vya uvuvi ili kuimarisha kazi za utafiti ambapo pai, Wizara inashirikiana na Taasisi ya utafiti kutoka Korea kuanzisha kituo cha majaribio ya utafiti wa mazao ya baharini.
Aidha, Taasisi ya utafiti ya mazao na rasilimali za bahari kutoka China imeshakubaliana na Wizara kuendeleza mambo mbali mbali katika shughuli za utafiti na ufugaji wa mazao ya baharini na kueleza kuwa hivi sasa wamo katika mchakato wa kuandaa mkataba juu ya uanzishwaji wa kituo cha utafiti wa baharini huko Pemba.
Uongozi huo ulieleza kuwa Wizara imeimarisha usimamizi wa rasilimali za bahari kwa kufanya doria katika maeneo ya hifadhi, kutoa mafunzo ya utunzaji wa mazingira kwa wavuvi na kufanya semina kwa viongozi wa serikali pamoja na mikutano kwa wavuvi.
Wizara ilieleza kuwa uzalsiahji wa samaki umeongezeka kutoka tani 28,758 mwaka 2011 mpaka tani 29,410 mwaka 2012 ambapo pia uzalishaji wa mwani nao umeongezeka kutoka tani 13,040 mwaka 2011 hadi tani 15,088 mwaka 2012 na kuongezeka usafirishaji wa mwani mkavu hadi kufikia tani 14,393 mwaka 2012. Sambamba na hayo, Wizara hiyo ilieleza kuwa jumla ya watu 30 wakiwemo wajasiriamali 18 na wafanyakazi 12 walihudhuria mafunzo ya mua mfupi ya ufugaji wa samaki nchini China.
Naye Dk. Shein kwa upande wake alitoa pongezi kwa Wizara hiyo kwa mafanikio makubwa iliyoyapata huku akiendelea kusisitiza haja ya viongozi wa Wizara kuwa na utamaduni wa kuzungumza na wafanyakazi wao juu ya masuala ya kazi hatua ambayo itaweza kuwaweka karibu na kusaidia kuimarisha ufanisi wa kazi.
Pamoja na hayom Dk. Shein alieleza haja ya viongozi kuweka utaratibu wa kuyazungumza mafanikio yao waliyoyapata kwa kupitia vyombo vya habari sambamba na kufanya mazungumzo na waandishi wa habari kwani ni utaratibu uliowekwa na serikali. Aidha, Dk. Shein alipongeza juhudi zinazochukuliwa na Wizara hiyo katika kupambana na uvuvi haramu katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba na kusifu mafanikio yaliopatika kwa wavuvi wa Chwaka na Marumbi.
Dk. Shein pia, alipongeza hatua ya Wizara ya kuanza utaratibu wa kusomesha wafanyakazi wake katika fani ya Pathology na kusisitiza kuendelezwa utamaduni huo wa kuwasomesha wataalamu katika fani nyeti kama hizo. Katika maelezo yake Dk. Shein alieleza kuwa huku Wizara hiyo ikitoa elimu kwa wakulima wa mwani pia, ipo haja ya kushirikiana na Wizara ya Biashara kuyashajiisha makampuni ya kununua bidhaa hiyo kuowafikia wakulima hao kwa kuwaongeza bei ya zao hilo wakulima hao.