Na Mwandishi Wetu
Rais Kikwete ashiriki kuchangisha upanuzi wa chuo Dar
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete usiku wa Aprili 13, 2013, ameshiriki katika shughuli ya kuchangisha kiasi cha Sh. Milioni 285 kwa ajili ya upanuzi wa Chuo cha Al-haramain cha Dar es Salaam.
Shughuli ya mchango huo ulioendeshwa wakati wa chakula cha jioni cha hisani kwenye Hoteli ya Serena, Dar Es Salaam iliandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kwa ajili ya kupata fedha za upanuzi wa Chuo cha Al-Haramain ambacho BAKWATA imeamua kukifanya Chuo Kikuu.
Kiasi cha Sh. Milioni 360 zilikuwa zinatafutwa kwa ajili ya upanuzi wa chuo hicho unaofanyika kwa awamu katika shughuli ya jana ambayo miongoni mwa watu wengine mashuhuri ilihudhuriwa na Rais Ali Hassan Mwinyi, Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Sheikh Issa Bin Shaaban Simba na Kadhi Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abdallah Mnyasi.
Jumla ya kiasi cha Sh. Milioni 800 zinahitajika kukamilisha mageuzi ya kukifanya Chuo cha Al-Haramain kilichoko kwenye ardhi kiasi cha ekari nane katika Jiji la Dar Es Salaam kuwa chuo kikuu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Kikwete aliwataka viongozi wa BAKWATA kuendelea na uchangishaji kwa sababu bado zinahitajika fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza uamuzi wa kukifanya Al-Haramain chuo kikuu, uamuzi ambao Rais Kikwete ameuelezea kama wa busara.
“Tuendelee kuchangisha. Kamati ya sasa imefanya kazi nzuri lakini nadhani tungeunda kamati nyingine kwa kuipanua ya sasa ili iwe na uwakilishi mpana zaidi na watu zaidi wa kusimamia uchangishaji huo,” alisema Rais Kikwete.
Ameongeza kuwa kamati hiyo na uchangishaji huo lazima ulenge watu wa dini zote kwa sababu BAKWATA “haichangishi Waislamu bali inachangisha jamii nzima kwa nia ya kuanzisha huduma kwa jamii nzima. Elimu ni kwa wote.”