MJI wa Geita na maeneo ya jirani juzi ulikumbwa na taharuki ya aina yake, pale mwanamke ambaye anadaiwa kwamba alifariki miaka mitano iliyopita alipoonekana akiwa hai katika eneo la Kasamwa. Inadaiwa kwamba Flora Onesmo (45) alifariki Februari 28, 2008 katika Hospitali ya Wilaya ya Geita na kuzikwa katika Kijiji cha Nakasenya, Kata ya Butundwe, lakini juzi alfajiri alikutwa ameketi nje ya nyumba ya dada yake aitwaye Monica James, anayeishi Kasamwa.
Aliyekuwa wa kwanza kumwona Flora ni mdogo wake aitwaye Monica Onesmo ambaye baada ya kuamka saa 11:00 alfajiri nyumbani kwa dada yake, alimwona mwanamke aliyekuwa ameketi nje ya nyumba hiyo, lakini alimfananisha mwanamama huyo na marehemu dada yake.
“Baada ya kumwona nilimwita mtoto wake tunayekaa naye na nikampigia simu dada (Monica) ambaye alikuwa amelala chumba kingine nikamwambia kwamba nimeamka na kumkuta mwanamke amekaa hapa nje, lakini kila nikimwangalia anafanana na marehemu dada yetu,” alisema Jubili na kuongeza kwamba alipowaita wote walitoka nje.
Alisema mtoto wa Flora (marehemu anayedaiwa kufufuka) anaitwa Rebeka Elisha (16) na kwamba walimchukua tangu 2008 wakati mama yake huyo alipofariki dunia katika Hospitali ya Geita ambako alikuwa amelazwa kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa ini.
Rebeka ambaye ni mtoto wa nne wa Flora alisema: “Mama mdogo alituita sisi tulikuwa tumelala akasema kwamba nje kuna mwanamke ambaye anafanana na marehemu mama yetu, ndipo na sisi tukatoka na kweli kumwangalia alikuwa ni yeye kabisa.”
Alisema walipomuhoji mama yake huyo kwamba ametokea wapi, aliwaeleza kuwa ametoka eneo la Katoro kwa mganga na aliletwa na watu ambao hakuwatambua Alhamisi saa 1:30 usiku ndani ya gari na watu hao walimshusha kwa mtu aitwaye Juma Luchunga ambaye ni jirani na dada zake hao.
Kauli ya Flora
Akizungumza na waandishi wa habari, Flora alisema yeye ni mkazi wa Katoro na kwamba alitokea Katoro nyumbani kwa mganga wa jadi ambaye hata hivyo hakumtaja kwa maelezo kwamba wataalamu wake (majini) wamemkataza.
“Nilikuwa naishi kwa mganga wa kienyeji ila alikuja mwanaume wakati nikiwa pale akaninywesha dawa kisha tukapakizwa kwenye gari na watu wawili ambao sikuwatambua, mmoja mwanamke na mwingine mwanaume mpaka hapa Kasamwa tukashushwa saa 1:00 jioni,”alisema Flora.
Alisema alipofika Kasamwa alikwenda kunywa uji kwa mama mmoja ambaye pia hakumtaja na kwamba baadaye alipelekwa nyumbani kwa mtu mwingine saa nne usiku, lakini watu wa nyumba hiyo walipomwona walimwambia: “Hapa si kwako twende tukupeleke kwa ndugu yako” na ndipo wakampeleka kwa dada yake ambako aliketi nje hadi alfajiri.
Flora alisema kabla ya kuishi kwa mganga alikuwa akiishi porini ambako alitupwa na watu asiowafahamu na baadaye aliokotwa na wasamaria wema ambao ndiyo walimpeleka kwa mganga ambako alikuwa akiishi muda wote.
CHANZO: www.mwananchi.co.tz