MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa wamesema “hawatakubali wala kuvumilia” hujuma dhidi ya chama chao. Viongozi hao kwa nyakati tofauti jana walisema hujuma hizo zimekuwa zikifanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Serikali ambayo imekuwa ikitumia vyombo vya dola na kwamba sasa wanapanga ugaidi wa kuwateka maofisa wa ngazi ya juu wa Chadema.
Suala la ugaidi liliibuka kwa nguvu katika wiki ya kwanza ya Bunge la Bajeti na sasa limehamia nje ya chombo hicho cha kutunga sheria kutokana na Chadema kuwatuhumu CCM na Serikali yake kwamba wanapanga njama za kuwateka maofisa wakuu wa chama hicho.
Jana Dk Slaa alipokuwa akimkaribisha Mbowe kufungua Mkutano wa Mafunzo na Mipango ya Vuguvugu la Mabadiliko ‘M4C’ na Kongamano la Katiba Mpya kwa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, alisema taarifa walizonazo zinaonyesha kuwa CCM ndiyo wanaofanya vitendo vya kigaidi wakishirikiana na Serikali.
“Tuna taarifa zote zinazoonyesha kwamba CCM ndiyo magaidi wakishirikiana na Serikali yake, lakini sisi tuko makini kuliko hata Serikali ya CCM na tuko makini kuliko hata Usalama wa Taifa na umakini huu ndiyo utakaotupeleka Ikulu mwaka 2015,”alisema Dk Slaa.
Hata hivyo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipotafutwa kujibu tuhuma hizo alisema hakuna jipya ambalo Chadema wamelisema.
“Kuna jipya katika hilo, ni yale yale ya kawaida na jana (juzi) Mwingulu alizungumza vizuri sana bungeni. Hiyo ni sawa na mchawi anapomwangia mtu na kufa anakuwa wa kwanza kwenda kulia msibani, nchi siku yoyotete haijengwi kwa ngonjera za maneno bali inajengwa kwa mipango,”alisema Nape.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima alipotakiwa kutoa msimamo wa Serikali juu ya tuhuma hizo alisema, “Mimi siwezi kuzungumza ila mtafute Waziri (Dk Emmanuel Nchimbi),”alisema Silima.
Alipotafutwa Dk Nchimbi kupitia simu yake ya mkononi, ilikuwa ikiita bila kupokewa.
Kauli ya Mbowe
Kwa upande wake Mbowe alisema, CCM imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali kuhakikisha inakisambaratisha chama hicho bila mafanikio.
“Watu wa Usalama wa Taifa wakishirikiana na CCM wamekuwa wakifanya mipango ya kutaka kuwateka maofisa wetu. Hawa watu ni wepesi sana na msiwaogope hata kidogo,”alisema Mbowe huku akishangiliwa na wanachama na makada waliofurika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Blue Pearl.
Mbowe alisema: “Ukiona chama chochote tawala kinatumia jeshi la polisi kutengeneza ushahidi wowote wa kihalifu hiyo ni dalili ya hatari kwa mustakabali wa usalama wa nchi.”
Mbowe alisema mbinu za sasa za CCM zinatokana na kushindwa kukivuruga chama hicho kwa propaganda kuwa ni chama cha familia, ukabila, ukanda na baadaye udini.
Katiba na Elimu
Kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, Mbowe alisema ikiwa itafika Aprili 30 mwaka huu bila hatua zozote kuchukuliwa, watamwamuru mjumbe wa tume hiyo kutoka Chadema, Profesa Mwesiga Baregu kujiondoa.
CHANZO: www.mwananchi.co.tz