Yanga, Oljoro Kuumana Mechi za Ligi Kuu Bara

Baadhi ya wachezaji Yanga

LIGI Kuu ya Vodacom inaendelea Aprili 13 mwaka huu kwa mechi mbili zitakazochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, na Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Yanga itakuwa mwenyeji wa Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa wakati Uwanja wa Sokoine utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Tanzania Prisons na Ruvu Shooting. Ligi hiyo itaendelea Aprili 14 mwaka huu kwa mechi kati ya wenyeji Azam na Simba. Mechi hiyo namba 155 itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

WASHELISHELI KUICHEZESHA AZAM CAF

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Shelisheli kuchezesha mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho kati ya Azam na AS FAR ya Morocco itakayofanyika Aprili 20 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Waamuzi hao ni Emile Fred atakayepuliza filimbi akisaidiwa na Steve Maire na Jean Ernesta. Mwamuzi wa mezani (fourth official) atakuwa Jean Claude Labrossa. Kamishna wa mechi hiyo ni Abbas Sendyowa kutoka Uganda.

Wakati huo huo, CAF imemteua Mtanzania Alfred Lwiza kuwa Kamishna wa mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho kati ya Liga Muculmana ya Msumbiji na Wydad Casablanca ya Morocco.

Mechi hiyo itakayochezwa kati ya Aprili 19,20 au 21 mwaka huu nchini Msumbiji itachezeshwa na waamuzi kutoka Zimbabwe wakiongozwa na Ruzive Ruzive.