JK Atia Saini Kitabu cha Maombolezo ya Bi. Margaret Thatcher

Mara baada ya kumaliza kutia saini Kitabu hicho, Balozi Melrose amemwambia: “Kwa niaba ya Serikali ya Uingereza na Watu wa Uingereza nakushukuru sana Rais kwa heshima hii ya kuja kutia saini Kitabu cha Maombolezo cha Margaret Thatcher. Waziri Mkuu wa nchi yetu atafurahi kujua kuwa umepata muda wa kuja kuungana nasi katika kuomboleza kifo hiki.”

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete Aprili 10, 2013 ametia saini Kitabu cha Maombolezo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Bi. Margaret Thatcher ambaye alifariki dunia Jumatatu wiki hii kwa ugonjwa wa kiharusi akiwa na umri wa miaka 87.
Rais Kikwete ametia saini Kitabu hicho kwenye Ubalozi wa Uingereza katika Tanzania ulioko Jengo la Umoja mjini Dar es Salaam.
Rais alikaribishwa kwenye Ubalozi huo na Balozi wa Uingereza katika Tanzania, Mheshimiwa Bi. Dianna Melrose na wafanyakazi wengine wa ubalozi huo na amekwenda moja kwa moja kutia saini kitabu hicho mara baada ya kuwasili kwenye Ubalozi huo.
Mara baada ya kumaliza kutia saini Kitabu hicho, Balozi Melrose amemwambia: “Kwa niaba ya Serikali ya Uingereza na Watu wa Uingereza nakushukuru sana Rais kwa heshima hii ya kuja kutia saini Kitabu cha Maombolezo cha Margaret Thatcher. Waziri Mkuu wa nchi yetu atafurahi kujua kuwa umepata muda wa kuja kuungana nasi katika kuomboleza kifo hiki.”
Naye Mheshimiwa Rais Kikwete amemjibu: “Kwa mara nyingine Balozi nakupa wewe binafsi, Serikali na watu wa Uingereza pamoja na familia ya Bi. Margaret Thatcher salamu zetu nyingi za rambirambi kufuatia msiba huu. Bi.Thatcher alikuwa kiongozi mashuhuri. Alikuwa kiongozi mwenye nguvu na msimamo na ndiyo maana anaheshimiwa na sisi sote.”
Bi. Margaret Thatcher alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza kwa miaka 11 kati ya 1979 na 1990. Alikuwa mwanamke wa kwanza na pekee mpaka sasa kushikilia nafasi hiyo na ndiye alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza kukaa madaraka kwa muda mrefu zaidi kuliko waziri mkuu mwingine yoyote katika kipindi cha miaka 150.