ALIYEKUWA Rais mteule wa Kenya, Uhuru Kenyatta leo ameapishwa rasmi kuwa Rais wa Kenya na kukabidhiwa madaraka na rais aliyemaliza muda wake, Mwai Kibaki. Kenyata amekula kiapo rasmi katika Uwanja wa Taifa la Kenya wa Moi Kasarani kwa kutumia biblia ambayo aliitumia Baba yake alipokuwa madarakani.
Kiapo cha Kenyata ambaye ni rais wa nne kimehudhuriwa na marais mbalimbali kutoka nchi jirani na Kenya, mabalozi, viongozi wa vyama na Serikali za nchi majirani na taifa hilo tajiri Afrika Mashariki. Kiongozi huyo alipigiwa mizinga 21 na Jeshi la Kenya (KDF) pamoja na kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa heshima kwa ajili ya hafla hiyo ya kihistoria.
Katika hafla hiyo Kibaki amemkabidhi vifaa vya kazi ikiwemo katiba ya nchi Rais mpya wa Kenya ikiwa ni ishara ya kukabidhi madaraka. Makamu wa Rais mpya wa Kenya, William Ruto pia ameapishwa rasmi ofisini na kukabidhiwa madaraka. Akizungumza katika hafla ya kiapo cha rais, Ruto alisema sasa si wakati wa Wakenya kujutia kura zao kwamba waliyemchagua hakushinda, bali ni wakati wa kuungana na kuangalia Serikali inatatuaje matatizo ya wananchi wake.
Alisema licha ya Kibaki kuondoka madarakani bado atakuwa tegemezi kwa kuendelea kuchota busara na ushauri kutoka kwake, kutokana na uhimara aliouonesha akiwa madarakani akiiongoza nchi ya Kenya. Alisema kazi yao kama viongozi wa Kenya ni kuhakikisha wanatekeleza ahadi ambazo walizitoa kwa wananchi wakati wakiomba ridhaa ya kuiongoza Kenya.
“…Sasa si wakati wa kulaumiana, bali ni wakati wa kuangalia nini Serikali mpya itafanya kukabiliana na changamoto kama za ajira, kupanda kwa bei ya bidhaa na masuala mengine muhimu kwa taifa.