Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda ameongoza mamia ya waombolezaji kuuaga mwili wa aliyekuwa Mhadhiri wa Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, na wakili maarufu Profesa Michael Wambali ambaye alifariki dunia Aprili 4, 2013 katika hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na majeraha aliyoyapata kwenye ajali ya gari. Shughuli ya kuuaga rasmi mwili wa marehemu Profesa Wambali ilifanyika leo, Aprili 8, 2013 kwenye ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kabla ya kupelekwa kanisani kwa misa maalum.
Akizungumza na waombolezaji hao kabla ya kutoa heshima za mwisho, Waziri Mkuu alisema mchango wa Prefesa Wambali kwenye fani ya sheria ni mkubwa mno na hauelezeki. “Kama walimu wenzake wangeamua kuhesabu idadi ya wanafunzi ambao Profesa Wambali aliwafundisha, ni dhahiri kuwa idadi yao ingekuwa kubwa kuliko tunavyoweza kufikiria,” alisema.
“Juzi tu tarehe 29 Machi, ametimiza miaka 59 ya kuzaliwa na siku sita baadaye akaaga dunia, lakini katika kipindi cha miaka yake 59 ni miaka 32 ambayo aliitumia hapa chuoni. Hapa tulipo wapo Majaji, Mawakili wa Serikali na wa kujitegemea, mahakimu na wengine wako mikoani wameshindwa kufika hapa leo… lakini wote hawa wamefundishwa na Prof. Wambali katika kipindi cha miaka 32 aliyokaa hapa chuoni,” alisema.
Alisema fani ya sheria imepoteza kiongozi makini na mfano wa kuigwa. “Tumepoteza kiongozi mzuri na makini siyo kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam peke yake bali ni kwa Tanzania yote,” aliongeza. Aliwasihi wanafamilia waikubali hali ya kuondokewa na mpendwa wao, wajipe matumaini kwamba mwenzao ametangulia na akawataka waendelee kumuombea kwa Mungu ili ampokee huko mbinguni.
Kwa wanafunzi wa wafanyakazi wa Shule Kuu ya Sheria, Waziri Mkuu alikuwa na haya ya kusema: “Ingawa Profesa Wambali ameondoka, ninaamini bado ataendelea kuwa nasi kwani ametuachia kazi zake nyingi za kimaandishi ambazo zitatumiwa na wengine katika siku zijazo. Tukienzi hilo, tutakuwa tunaendeleza yale aliyokuwa akiyasimamia.”
Naye Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk. Asha-Rose Migiro ambaye aliwahi kufanya kazi na Profesa Wambali miaka ya 80, wakati akitoa nasaha zake alisema alifanya naye kazi ofisi moja na waliwahi kufundisha masomo ya aina moja.
Dk. Migiro alisema kila aliyewahi kuwa mwanafunzi wa Prof. Wambali hawezi kuacha kumkumbuka. “Hatuwezi kumrudisha kwa sasa ila kila aliyewahi kuwa mwanafunzi wa Profesa Wambari atamkumbuka daima. Mike ameondoka lakini atabakia mioyoni mwetu. Kila tutakapoona familia yake ama kuona kuona kazi zake za taaluma, tutaendelea kuonana naye,” alisema.
Waziri Mkuu amewasili mjini Dodoma mchana huu kuhudhuria mkutano wa 11 wa Bunge unaotarajiwa kuanza Jumanne, Aprili 9, 2013.