Ujue Wajibu wa Kijana…!

Wajibu wa kijana Tanzania

Wajibu wa kijana Tanzania…!

KIJANA ni lazima ujitambue na kujitambua kwako kuwe na tija kwa jamii na taifa lako hiyo itasaidia kuongeza hadhi ya vijana kwa jamii. Vijana sio tena taifa la kesho bali taifa la leo na sasa kwani ndio wenye nguvu na ubongo unaoweza kutafakari mambo na kuyapatia ufumbuzi sahihi lakini pia vijana ndio nguzo ya maendeleo.

Wewe kama kijana hebu jiulize unafanya nini ili kuchangia mabadiliko katika jamii yako? Je huchangii chochote kwa sababu hutaki au hakuna nyenzo wala vyanzo? Je nani alipaswa kuandaa mazingira ya kijana kuwa chachu ya maendeleo? Je kijana wa leo umeandaliwaje kielimu ili kukabiliana na changamoto za maisha?

Ukitafakari hayo na mengine utagundua kijana unawajibu mkubwa sana wa kuleta mabadiliko kwa jamii yako lakini je ni mabadiliko gani unapaswa kuyaleta na uanzie wapi?

Kwanza kabisa kijana unapaswa kushiriki kuleta mabadiliko ya kimfumo ili kuhakikisha mfumo uliopo unasimamia rasilimali za nchi kwa manufaa ya wananchi ikiwemo wewe(kijana) ambaye leo unaonekana balaa kwa sababu kwa kukosa elimu umekosa ajira na huna mtaji tena kwa sababu hata ule mtaji uliokuwa unautumia kuendeshea biashara ndogondogo wamekuja na kuuharibu wote kwa kukufukuza kwenye eneo la biashara bila kuonesha wapi uende (mf. Ubungo).

Ili kuhakikisha tunayaleta mabadiliko ni kujitoa kwa moyo wote kusema imetosha na kuhakikisha tunamiliki na kuitunza kadi ya kupigia kura kwa sababu hiyo inathamani kubwa linapokuja suala la kuamua juu ya nani umkabidhi asimamie rasilimali zinazokuzunguka ili zilete manufaa kwako na jamii kwa ujumla.

Ni vyema basi kama kijana ukajihoji mwenyewe kama je unataka mabadiliko au hali iliyopo inakutosha? Ni lazima ujiulize rasilimali zilizopo zinakunufaisha au la na je zinamnufaisha nani? Je uliowapa dhamana ya kusimamia rasilimali wanakwambia nini juu ya hali ngumu ya maisha,mateso unayofanyiwa au wanayofanyiwa ndugu zako waliozungukwa na madini au wanyama pori kama kule mwadui,Geita na Ngorongoro.

MIMI 2015 SIKUBALI TENA KUCHAGULIWA MTU WA KUNIONGOZA NI LAZIMA NISHIRIKI KUCHAGUA ILI NIFANYE UAMUZI SAHIHI KWANI NIMETAMBUA KURA YANGU MOJA INAWEZA KULETA MABADILIKO MAKUBWA