Dk. Mwakyembe Kuliangalia Umpya Ongezeko la Nauli za Mabasi, Daladala
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe amewaahidi wananchi kuhakikisha analifuatilia suala la ongezeko la nauli mabasi na daladal kwa kina ili kuangalia viwango vilivyopangwa vinaweza kulipwa na kada yote ya wananchi.
Hata hivyo amesema kwa kipindi hiki ambacho anafuatilia suala hilo, nauli katika treni zinazotoa usafiri jijini Dar es Salaam, yaani ile ya TAZARA na ya Ubungo hazitapandishwa kama itakavyokuwa kwa daladala ili kutoa hauweni kwa baadhi ya abiria.
Waziri Dk. Mwakyembe ametoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza katika maadhimisho ya Media Day yaliyofanyika kwenye viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam. Akifafanua zaidi kuhusiana na suala la kupanda kwa nauli, alisema amepata habari hizo za akiwa nje ya ofisi hivyo hawezi kulizungumzia kwa kina lakini aliomba apewe muda ili apate taarifa rasmi ofisini na kuangalia namna ya kulishughulikia.
Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha bei zote za viwango vya nauli zinazopangwa zinaweza kulipwa na kila mwananchi na si kuwa mzigo kwake. “Binafsi nimelisikia suala hilo la kupanda kwa nauli nikiwa nje ya ofisi (nilikuwa jimboni kwangu kulikuwa na mafuriko) naombeni nipewe muda nilipate ofisini na kuangalia nini cha kufanya,” alisema Dk. Mwakyembe.
Dk. Mwakyembe aliulizwa swali hilo la kutakiwa kutoa msimamo wake kama waziri wa uchukuzi na wanahabari mara baada ya kumaliza kutoa hotuba yake katika hafla hiyo ya wanahabari alipokuwa mgeni rasmi wa shughuli hiyo.
Awali akitoa hotuba yake alisisitiza apanii kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao, lakini lengo lake ni kuchapa kazi kiufasaha ili aje kuwa miongoni mwa mawaziri bora Serikalini. Dk. Mwakyembe ni miongoni mwa mawaziri machachari na wachapakazi katika Serikali ya Tanzania anayefanya kazi na kuungwa mkono na kuwavutia wengi kiutendaji.