Na Hussein Makame na Frank John-Maelezo
CHAMA cha Madaktari Bingwa wa Upasuaji Tanzania (TSA) kimewaomba wananchi wa mikoa ya Kilimanjaro na Arusha na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kupata huduma za uchunguzi na upasuaji wa magonjwa mbalimbali bure.
Huduma hiyo itatolewa bure kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na chama hicho, ambapo madaktari bingwa wa upasuaji wanatarajiwa kutoa huduma hizo kwa wananchi wa maeneo hayo.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa chama hicho, anayemaliza muda wake Dk. Kitungi Nungu wakati alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Dk. Nungu alisema uchunguzi na upasuaji huo utatolewa kwa magonjwa ya mifupa, tumbo, matatizo ya njia ya haja ndogo na magonjwa ya kina mama katika hospitali za mount Meru, Mbulu, Hydom, Machame na Babati.
Alisema huduma hiyo, itaanza kutolewa kuanzia Aprili 11 hadi 16 mwaka huu ambapo kila hospitali itakuwa na madaktari bingwa wasiopungua watano kwa ajili ya kutoa matibabu hayo kwa wakazi wa maeneo ya karibu na hosipitali hizo.
Kwa upande wake Mwenyekiti mtarajiwa wa chama hicho, Dk. Paul Marealle alisema huduma hiyo itafuatiwa na mkutano mkuu wa chama hicho na ule wa madaktari bingwa wa Afrika Mashariki,Kati na Kusini mwa Afrika.
Aidha Dk. Nungu alifafanua kuwa mkutano huo utafanyika katika hoteli ya Snow-Crest iliyoko jijini Arusha kuanzia Aprili 17 hadi 19 mwaka huu, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Kaulimbiu ya mkutano huo itakuwa ni ‘Ufundishaji wa Daktari Bingwa wa Upasuaji kwa Leo na Kesho’. Katika mkutano huo madaktari hao watajadili jinsi ya kumpata madaktari bingwa ili kukabiliana na uhaba wa wataalamu hao nchini.