WAFANYAKAZI Benki ya Posta Kunufaika na Mfuko wa Kufarijiana

Mwenyekiti wa Mfuko wa Kufarijiana wa Benki ya Posta Tanzania, Bw. Iddi Kibwana akizungumza katika Mkutano Mkuu. Kulia ni Katibu wa Mfuko Bw. Andrew Chimazi.

WAFANYAKAZI wa Benki ya Posta Tanzania, wataendelea kunufaika na mfuko wao uitwao “Mfuko wa Kufarijiana” , unaowawezesha wafanyakazi kupata mafao mbalimbali pindi wanapofikwa na tatizo. Mfuko huo unaoendeshwa na wafanyakazi wote wa Benki ya Posta kama wanachama, ulianzishwa mwaka 1995 ukiwa na lengo la kumfariji na kumsaidia mfanyakazi pindi anapopata tatizo kama vile kifo, majanga , ugonjwa n.k. Mfuko huo unatunishwa kila mwezi kwa makato kutoka kwenye mishahara ya wafanyakazi ya kila mwezi.

Akizungumza kwenye kikao cha wafanyakazi cha mfuko huo kinachofanyika kila baada ya miaka minne, Mwenyekiti wa mfuko huo wa Benki ya Posta Iddi Kibwana alisema uongozi wa mfuko umepanga mikakati mizuri ya kuuboresha mfuko huo, ili wafanayakazi waendelee kufaidika nao. Aliwakumbusha wanachama wa mfuko huo kwamba japo katiba ya mfuko huo inaupa uongozi wa mfuko mamlaka ya kufanya mabadiliko mabali mbali na maboresho ya mfuko, wao kama wafanachama wanajukumu la kuridhia marekebisho hayo. Mbali na kupitisha marekebisho mbalimbali kwenye mfuko huo, pia mkutano huo ulifanya uchaguzi na kupata viongozi wa mfuko watakao ongoza mfuko huo katika miaka minne (4) ijayo.

Mkurugenzi wa Rasilimali watu wa benki ya Posta Peter Mapigano, alichukua furasa ya mkutano huo kuwasifu waasisi wa mfuko huo ambao umeonesha kuwa faraja kubwa kwa wafanyakazi. Alisema kwamba benki ya posta kama muajiri hawezi kutatua matatizo yote ya wafanyakazi wake japo angapenda kufanya hivyo, hivyo mfuko huo ni suluhisho la matatizo mengi ambayo muajiri kwa namna moja au nyingine hawezi kuyatekeleza.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta Sabasaba Moshingi aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo, aliwaasa wafanyakazi wote kuendelea kuchangia mfuko huo kwani mbali na kuwanufaisisha, pia unajenga umoja na upendo miongoni mwa wafanyakazi.

Aliwashauri viongozi wapya waliochaguliwa kupanua wigo wa mfuko huo kwa kuangalia maeneo mengine yanayoweza kuchangiwa kama vile kutoa zawadi kwa wanachama wanao oana, zawadi kwa mtoto aliyezaliwa,kuangalia uwezekano wa kuongeza viwango vya kuchangia ili kuhimili ongezeko la faraja na pia Kuangalia uwezekano wa kuruhusu wafanyakazi wanao acha kazi endapo wanahitaji kuendelea kuwa wanachama, waruhusiwe kuendelea kuchangia ili waendelee kupata faraja kama wengine.