JK WAKATI WA MAADHIMISHO YA SIKU YA KILELE CHA MIAKA 60 YA BARAZA LA UUGUZI NA UKUNGA TANZANIA, VIWANJA VYA MNAZI MMOJA, DAR ES SALAAM, TAREHE 19 MACHI, 2013
Mheshimiwa Dkt. Seif Seleman Rashid (Mb), Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii;
Mheshimiwa Said Meck Sadik, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Dkt. Khadija Malima, Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga, Tanzania;
Viongozi na Watendaji Wakuu wa Serikali Mliopo Hapa;
Wawakilishi wa Washirika wa Maendeleo na Wadau wa Afya;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana:
Awali ya yote niruhusuni nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa siku ya leo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja. Nakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, Mwenyekiti na viongozi wenzako wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania kwa kunishirikisha kwenye sherehe hii adhimu ya kuadhimisha miaka 60 ya uhai wa Baraza la Uuguzi na Ukunga hapa nchini. Kipindi cha miaka 60 siyo kifupi, ingekuwa Baraza la Uuguzi na Ukunga ni mtumishi wa umma, kwa sasa ungekuwa ni muda wake wa kustaafu. Na, kama angekuwa mwanadamu angekuwa babu au bibi mwenye wajukuu na kukaribia kupata vitukuu. Lakini kwa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, hivyo sivyo. Halijazeeka bali ndiyo limekomaa na wala halijachoka na bado lina nguvu na linasonga mbele kwa, ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi. Hongereni sana.
Ndugu Wauguzi na Wakunga;
Kwa namna ya kipekee nawapongeza viongozi wa Baraza la Wauguzi na Wakunga kwa kazi nzuri ya kuandaa maadhimisho haya. Hakika yamefana sana. Maonyesho yalikuwa mazuri sana. Yameeleza vizuri kazi wazifanyazo Wauguzi na Wakunga na mafanikio mliyopata. Aidha, risala yenu ilikuwa nzuri, imeeleza kwa kina mafanikio mliyopata na changamoto zinazowakabili ambazo mngependa tuzijue na kusaidia kuzipatia ufumbuzi. Napenda kuwahakikishia kuwa yote mliyosema katika risala tutayafanyia kazi. Bahati nzuri mengi tunayafahamu na hatua mbalimbali zimechukuliwa na zinaendelea kuchukuliwa kuyapatia ufumbuzi. Nitatafuta nafasi katika muda si mrefu tukutane na viongozi wa Baraza tuzungumze kwa kina na utulivu masuala yahusuyo Wauguzi na Wakunga nchini.
Vile vile nalipongeza sana Baraza la Uuguzi na Ukunga nchini kwa juhudi zao walizozifanya na wanazoendelea kufanya kuhakikisha kuwa taaluma ya uuguzi na ukunga inasonga mbele. Leo tumekusanyika hapa kujivunia mafanikio ya kutia moyo yaliyotokana na juhudi zenu. Aidha, nawapongeza watu na wadau mbalimbali ambao kwa namna moja au nyingine wametoa mchango mkubwa kuanzisha na kuimarisha taaluma hii hapa Tanzania. Michango yao haitasahaulika kamwe katika taaluma ya uuguzi na ukunga nchini, tutaienzi daima.
Ndugu Mwenyekiti;
Nimevutiwa sana na Kauli Mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inayosema “Taaluma ya Uuguzi na Ukunga inasonga mbele: Ilikotoka, hali ya sasa na hali ya siku za usoni”. Ni Kauli Mbiu iliyobeba ujumbe maridhawa kabisa. Inatukumbusha umuhimu wa kujitathmini wenyewe kwa kuangalia safari yetu, tangu tulipoanza enzi ya mkoloni, tulipo sasa na namna ya kutumia uzoefu wa miaka 60 kusonga mbele kwa lengo la kufanya vizuri zaidi siku za usoni. Hivyo ndiyo ilivyo kwa historia yetu sisi binadamu. Huwezi kubaki hapo ulipo miaka yote, lazima kubadilika na wakati kwa kuzingatia changamoto zilizopo. Ni lazima kuendelea kuboresha pale kwenye upungufu kwa nia ya kufanya vizuri zaidi kadri siku na miaka inavyoenda. Hivyo na sisi tunategemea Kauli Mbiu ya madhimisho ya mwaka huu itakuwa chachu ya kuimarisha na kuboresha zaidi taaluma ya uuguzi nchini siku za usoni. Bila shaka mtaweza!
Ndugu Wananchi;
Tangu nchi yetu imepata Uhuru, Serikali imekuwa ikishirikiana kwa karibu sana na Baraza la Uuguzi na Ukunga kuendeleza taaluma hiyo. Tumekuwa tukifanya hivyo kwa vile tunatambua na kuthamini mchango mkubwa na muhimu unaotolewa na Wauguzi na Wakunga katika kuboresha afya za wananchi. Wauguzi na Wakunga ni moja ya nguzo kuu katika utoaji wa huduma ya afya. Kazi ya daktari haikamiliki bila ya kuwepo Muuguzi. Wakati mwingine wamekuwa wakisaidia kutoa huduma ya afya katika maeneo mengi nchini ambayo yana uhaba wa madaktari. Wakunga hawana badala yao. Bila ya Wakunga uzazi huwa na mashaka na vifo vya kina mama na watoto huwa vingi. Kukosekana kwa Wakunga wa kutosha ni moja ya sababu ya vifo vya kina mama kwa matatizo ya uzazi. Ninaposema hivyo sina maana kuwa wakunga wa jadi hawafai, la hasha, wengi tulizaliwa mikononi mwao na tunaishi. Hata hivyo, upeo wao wa ufahamu ni mdogo. Ilikuwa sawa wakati ule, lakini hatuna sababu ya kuendelea hivyo.
Ni ukweli ulio wazi kwamba tuna upungufu mkubwa sana wa Wauguzi na Wakunga kama ilivyo kwa Madaktari na Waganga wa ngazi mbalimbali. Hapa nchini Daktari mmoja anatakiwa kuhudumia watu 50,000 na muuguzi mmoja kwa ajili ya watu 23,000. Jawabu lake lipo kwenye kufundisha na kuajiri Madaktari na Wauguzi wengi. Tumekuwa tunajenga vyuo vipya na kupanua vilivyopo ili kutoa mafunzo kwa watu wengi zaidi. Kazi hiyo inafanywa na Serikali na wadau wengine. Matokeo yake ni kuongezeka sana kwa idadi ya Wauguzi na Wakunga kama mlivyosema kutoka chini ya 100 mwaka 1953 hadi 31,000 sasa. Lakini bado pengo ni kubwa. Nawahakikishia kuwa tutaendelea kupanua fursa za mafunzo.
Ndugu Wananchi;
Sera mpya ya Afya ya mwaka 2007 na Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi vina lengo la kuongeza idadi ya Wakunga na Wauguzi na kukabili matatizo hayo. Vile vile kuongeza vifaa na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi.
Ndugu Mwenyekiti;
Ndugu Wauguzi na Wakunga;
Nalipongeza Baraza kwa kusisitiza weledi wa kazi ya uuguzi na ukunga. Nakubaliana nawe kuhusu kupambana na wauguzi bandia na vyuo visivyokuwa na viwango stahiki vinavyotoa wauguzi wasiokuwa na sifa stahiki. Naungana nawe kuhusu umuhimu wa Wauguzi kuzingatia maadili ya taaluma yenu katika utendaji wa shughuli zenu za kila siku. Muuguzi na Mkunga wazingatie upendo, uadilifu, huruma na uwajibikaji wakati wote wanapotoa huduma za uuguzi na ukunga. Fanyeni kazi kwa bidii na maarifa ili kuboresha zaidi utendaji wenu. Kumbukeni kuwa wateja wenu muda wote wanakuwa kwenye maumivu ya kimwili au ya kimawazo. Hivyo wanategemea kupata huduma itakayotolewa kwa wakati muafaka na kwa upendo na huruma. Msipofanya hivi, mtawazidishia wagonjwa maumivu na wakati mwingine kukatisha maisha yao pasipostahili.
Yapo malalamiko mbalimbali na tuhuma za wagonjwa kunyanyaswa, kunyimwa huduma na kuombwa rushwa na baadhi yenu. Inasikitisha zaidi kusikia kuwa mara nyingi watu wanaofanyiwa vitendo hivyo vya kikatili ni wagonjwa wenye uwezo mdogo wa fedha. Wanakwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vilivyo chini ya Serikali wakidhani ni kimbilio la wanyonge, wanakutana na dhahama ya Wauguzi na Wakunga wasio waaminifu. Sisemi wote, lakini wapo baadhi yenu ambao wanafanya vitendo hivyo viovu.
Ndugu Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania;
Nimevutiwa na msimamo wa Baraza wa kutokuafiki tabia hiyo. Naomba Baraza la Uuguzi na Ukunga kuyafanyia kazi haraka malalamiko hayo pindi yanapotokea. Ikithibitika wahusika wachukuliwe hatua za kinidhamu na ikiwezekana wapelekwe kwenye vyombo vya sheria. Fanyeni taaluma ya uuguzi na ukunga iwe taaluma ya wito kama inavyotakiwa iwe. Wekeni utaratibu mzuri wa mgonjwa kumtambua kwa urahisi Muuguzi au Mkunga aliyemhudumia na kutoa maoni yake kwa urahisi. Mkifanya hivyo, itakuwa rahisi kuwathamini Wauguzi na Wakunga hodari na kuwaadhibu wale wasio waaminifu na wazembe. Tofauti na hivyo, mtashindwa kukidhi matarajio ya wananchi na kupoteza imani ya wale mnaowahudumia.
Mimi na wenzangu Serikalini tunawahakikishia kuwa tutaendelea kushirikiana nanyi kwani Wauguzi na Wakunga wakifanya vizuri, malengo ya Serikali ya kuboresha afya za Watanzania yatakuwa yamefikiwa. Tutaendelea kuboresha bajeti ya sekta ya afya na maslahi ya Wauguzi na Wakunga kadri hali itakavyokuwa inaruhusu. Tutatoa kipaumbele kwa Wauguzi na Wakunga wanaofanya kazi katika maeneo ya mijini na vijijini kwa kuwajengea makazi bora ili kupunguza adha wanayopata ya ukosefu wa nyumba. Vile vile tutaendelea kuimarisha na kupanua fursa za mafunzo ya Wauguzi na Wakunga na kuwapatia ajira wanapohitimu mafunzo yao. Tumeanza kufanya hivyo kwani katika Chuo Kikuu cha Dodoma tumeanzisha Chuo cha Tiba ambapo tayari kuna wanafunzi 325 wanaosomea Shahada ya Uuguzi na Ukunga. Tutaendelea kupanua fursa za mafunzo kadri ujenzi wa chuo utakavyokuwa unaendelea.
Mheshimiwa Waziri;
Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania;
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu, naomba nirudie kukushukuru wewe Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, kwa kunialika kuja kushiriki nanyi katika sherehe hii. Nawapongeza sana Wauguzi na Wakunga kwa mafanikio makubwa mliyofikia leo . Naomba muongeze juhudi zaidi kwani safari bado ni ndefu. Mimi na wenzangu Serikalini tutaendelea kutoa ushirikiano unaostahili ili taaluma ya uuguzi na ukunga izidi kushamiri na kutoa huduma tunayotarajia.
Mwisho nawashukuru wananchi wote kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye siku ya kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania. Nawatakia Wauguzi na Wakunga popote walipo nchini Tanzania kila la heri na mafanikio tele katika utendaji wa shughuli zenu.
Asanteni.