HOTUBA YA RAIS KIKWETE –KATIKA SHEREHE ZA UZINDUZI WA CHUO CHA MAFUNZO YA TEHAMA VETA KIPAWA DSM
Mheshimiwa Dk. Shukuru Kawambwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi;
Mheshimiwa Saidi M. Sadiki Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Mheshimiwa Young-Hoon Kim Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania;
Prof. Idrissa B. Mshoro Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi;
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Mhandisi Zebadia Moshi;
Viongozi na Watendaji wa Serikali Mliopo Hapa;
Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana:
Awali ya yote nakushukuru Mhe. Waziri Kawambwa na uongozi wa VETA kwa kunialika kuja kushiriki kwenye uzinduzi wa chuo cha mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hapa VETA Kipawa. Hakika hii ni faraja kubwa kwangu kupata fursa hii ya kuzindua rasmi Chuo hiki maalum cha TEHAMA.
Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wananchi wote kwa ujumla, napenda kutoa shukrani za pekee kwa Mhe. Park Geun-hye, Rais wa Jamhuri ya Korea, Serikali na watu wake kwa msaada wao mkubwa uliowezesha kujengwa kwa chuo hiki. Hatuna neno zuri la kushukuru isipokuwa kusema asanteni sana. Namuomba Balozi Youn-Hoon Kim wa nchi hiyo azifikishe salamu zetu za shukrani. Please convey our deepest appreciation and gratitude to Her Excellency the President, the Government and people of the Republic of Korea. We thank you for your generosity.
Ndugu Wananchi;
Ujenzi wa chuo hiki ni sehemu ya jitihada za Serikali za kupanua fursa za elimu kwa vijana wetu na Watanzania kwa jumla hapa nchini. Pamoja na elimu ya msingi, sekondari na chuo kikuu, tumetoa kipaumbele kwa elimu ya ufundi. Kwa upande wa elimu ya ufundi, mpaka sasa vipo vyuo vya ufundi stadi 750 hapa nchini vyenye wanafunzi 121,348. Kati ya hivyo, vinavyomilikiwa na VETA ni 27. Leo tunazindua chuo kingine cha VETA. Uzuri wa vyuo vya ufundi ni kwamba vinawaandaa wahitimu kujiajiri wenyewe na hivyo kusaidia kupunguza tatizo la ajira.
Chuo tunachokizindua leo ni cha aina yake katika vyuo vya ufundi vya VETA. Tulizoea kuwa na vyuo vya kutoa mafunzo ya ufundi wa umeme, ujenzi, kushona, bomba n.k. TEHAMA haikuwepo katika fikra na mipango ya VETA. Lakini wakati umebadilika, hivi sasa teknolojia ya habari na mawasiliano ndiyo nyenzo kuu katika kuendesha shughuli za biashara, utawala, utendaji viwandani pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali ikiwemo elimu na mafunzo mbalimbali. Mahitaji na matumizi ya TEHAMA yanazidi kuongezeka na kupanuka siku hadi siku na yanagusa takriban shughuli zote za maendeleo: biashara, uchumi na utawala. Hata maisha binafsi ya watu yanaguswa na TEHAMA. Hii ni kweli duniani na hata katika nchi yetu. Mahitaji hayo yameongezeka sana kuliko ilivyokuwa siku za nyuma.
Mabibi na Mabwana;
Kwa kutambua ukweli huo, Serikali imeamua kuchukua hatua za makusudi kuendeleza taaluma na matumizi ya TEHAMA nchini. Mikakati inafanywa ya kupanua mafunzo ya kompyuta na teknolojia ya habari katika ngazi ya sekondari, vyuo vya ufundi na elimu ya juu. Napenda kutoa pongezi maalum kwa Bodi ya Taifa ya Mafunzo ya Ufundi Stadi na uongozi wa VETA kwa uamuzi wao wa kujumuisha mafunzo ya teknolojia ya habari katika mitaala ya ufundi stadi ya vyuo vya VETA. Hatua hiyo itasaidia kuliwezesha taifa kupata waaalamu wa fani hii muhimu.
Niruhusuni niwashukuru kwa namna ya pekee marafiki zetu wa Korea Kusini kwa msaada mkubwa waliotupatia wa kujenga chuo hiki cha TEHAMA hapa Kipawa. Wametusaidia sana kujenga uwezo wa kufundisha na kupata wataalamu zaidi wa TEHAMA nchini watakaoendeleza matumizi ya TEHAMA kwenye maeneo mbalimbali kama vile elimu (e-learning, on line education), biashara (e-commerce), afya (tele-medicine) na maswala ya utawala (e-government).
Ndugu Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi;
Chuo hiki ni hazina kubwa katika maendeleo ya nguvu kazi ya TEHAMA hapa nchini. Ni matarajio yangu kuwa Bodi na menejimenti mtahakikisha kuwa, Chuo hiki kinatumika vizuri ili kupunguza upungufu wa wataalamu wa TEHAMA. Napenda kuona mafunzo ya namna hii yanatolewa kwa vyuo vyote vya VETA. Tukifanya hivi, tutawafikia Watanzania wengi zaidi.
Mheshimiwa Waziri;
Naomba nimalizie kwa kurudia kutoa pongezi zangu kwa Wizara yako kwa jitihada mnazozifanya katika kusaidia kupanua na kukuza mafunzo ya ufundi katika taifa letu. Nawapongeza pia wenzetu wa VETA kwa kusimamia vizuri mafunzo ya ufundi. Ongezeni bidii ili vijana wanaopata mafunzo kwenye vyuo vyenu wazidi kuongezeka na waendelee kugombewa kwenye soko la ajira. Vile vile muimarishe mafunzo ya ujasiriamali ili vijana wanapohitimu waweze kujiajiri wenyewe.
Mwisho nawashukuru tena Serikali ya Jamhuri ya watu wa Korea kwa kutoa mkopo wa riba nafuu kwa ajili ya ujenzi na kutoa vifaa kwa vyuo vya Lindi, Manyara na Pwani. Nawashukuru pia wadau wengine, ikiwa ni pamoja na uongozi wa Halmashauri ya Ilala na wananchi wa Kipawa, kwa ushiriki wao katika kufanikisha ujenzi wa chuo hiki. Wito wangu kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam ni kuwa mkilinde, mkitunze na kukitumia kwa ukamilifu chuo hiki kwa maslahi ya taifa.
Asanteni kwa kunisikiliza.