Tanapa kuwashindanisha wanahabari, vyombo vya habari

Baadhi ya wahariri wa vyombo anuai vya habari wakiwa na viongozi wa juu wa TANAPA.

Na Joachim Mushi, Morogoro

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeanza kuwashindanisha waandishi wa habari pamoja na vyombo vya habari kuripoti taarifa mbalimbali za mbuga hizo ikiwa ni mkakati wa kuzitangaza mbuga hizo ambazo zimekuwa na mchango mkubwa kwa taifa.

Kauli hiyo imetolewa jana mjini hapa na Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Alan Kijazi alipokuwa akifungua warsha ya Jukwaa la Wahariri iliyoandaliwa na shirika hilo, ikiwa ni moja ya mikakati ya kujenga ushirikiano kati ya vyombo vya habari na Shirika la Hifadhi za Taifa.

Alisema vyombo vya habari vinanafasi kubwa ya kuweza kutangaza shughuli mbalimbali zinazofanywa na TANAPA kwa wananchi, hivyo kuelewa umuhimu wa kuhifadhi hifadhi za taifa kulingana na umuhimu na mchango wake katika mapato ya Serikali.

Aidha alisema kuanzia leo TANAPA itakuwa ikifuatilia kazi mbalimbali zinazofanywa na waandishi, wahariri, pamoja na vyombo vyao katika kutoa taarifa mbalimbali za kuelimisha jamii na umuhimu wa hifadhi za taifa, na baadaye itakuwa ikiwazawadia makundi yote hayo walioongoza katika kutoa taarifa hizo.

“TANAPA inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaofanywa na vyombo vya habari katika kuelimisha jamii umuhimu wa hifadhi za taifa, hivyo vyombo vya habari vina kila sababu ya kuendeleza kazi hii hasa kutoa taarifa chanya…endapo vyombo vya habari vitaamua kwa pamoja kutangaza utalii na kupiga vita uangili tutafanikiwa kwa kiasi kikubwa,” alisema mkurugenzi huyo.

“Sasa tunaanza programu maalumu ya kuvizawadia vyombo vya habari, tutatoa zawadi kwa vyombo vya habari, mwandishi mmoja mmoja na hata mhariri ambao wataonekana kufanya vizuri katika kuzitangaza mbuga zetu,” alisema Kijazi.

Akifafanua zaidi alisema utalii umekuwa ukichangia asilimia 17.2 katika pato la taifa, ukiachilia mbali faida nyingi na muhimu zinazopatikana katika suala zima la kuhifadhi mazingira, hivyo kumtaka kila Mtanzania kuwajibika juu ya utunzaji hifadhi na mazao yake.

Aliongeza pia suala la ujangili limekuwa likiongezeka kwa kasi katika mbuga mbalimbali za hifadhi ya taifa na endapo kila raia atatambua umuhimu wa hifadhi na kushiriki katika kuinda na kuhifadhi ujangili utapungua na hata kuondoka kabisa hivyo taifa kuendelea kunufaika na mapato ya utalii.

Warsha ya wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari iliyoanza jana mjini Morogoro, kwa wahariri kupewa mada anuai kutoka kwa wataalamu wa TANAPA inaendelea leo, ambapo wahariri watapata fursa ya kutembelea Hifadhi ya Mikumi na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanyika ndani ya eneo hilo.