Mshindi wa kiti cha uraisi katika uchauguzi mkuu wa Kenya kupitia muungano wa Jubilee, Uhuru Kenyatta amepingwa rasmi jana mbele ya Mahakama ya Juu ya Kenya Jumamosi. Raila Odinga wa muungano wa Cord ambaye alishika nafasi ya pili katika uchaguzi huo ulifanyika Machi 4, 2013, amewasilisha pingamizi lake mahakamani akitaka matokeo ya uchaguzi yatenguliwe.
Mahakama ya Juu ya Kenya inatarajiwa kutoa uamuzi juu ya pingamizi hilo katika kipindi cha siku 14. Kenyatta ambaye alitangazwa mshindi na Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ni mtoto wa Raisi wa kwanza wa nchi hiyo Jomo Kenyatta huku Raila Odinga ni mtoto wa aliyekuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Jaramogi Odinga akiwa namba mbili katika utawala wa Kenyatta.
Cord ilisema kwamba kwa kuwasilisha pingamizi lake ina uhakika kwamba matokeo ya uchaguzi huo yatatenguliwa. Wakili Kiongozi wa Cord, George Oraro alisema kwamba wana ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai yake mbele ya Mahakama ya Juu. ’’Sisi (Cord) tuna kesi ya kutafuta haki na tunafanyakazi kwa bidiii kubatilisha uamuzi wa IEBC iliyomtangazo Uhuru Kenyatta kuwa Rais Mteule,’’ Oraro alisema Jumamosi. Alisema tume hiyo haijatoa taarifa zote ambazo Cord inazihitaji lakini inao ushahidi wa kutosha wa kuweka pingamizi. Aliwataja wahusika katika kesi hiyo kuwa ni pamoja na Mwenyekiti wa IEBC,Isaack Hassan,Uhuru Kenyatta na Makamu wa Rais Mteule, William Ruto.
Mwisho
Na Isaac Mwangi, EANA