MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na wanaharakati wa masuala ya haki na usawa wa Kijinsia, haki za Binadamu, Demokrasia, Utawala bora na Maendeleo (FemAct), wanaharakati ngazi ya jamii, washiriki wa Semina za Jinsia na Maendeleo za kila Jumatano(GDSS) na wanachama wa Vituo vya Taarifa na Maarifa katika mikoa ya Mbeya, Morogoro, Shinyanga na Pwani tunafuatilia kwa umakini mchakato mzima wa kuandaa katiba mpya.
Kutokana na hili, taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba (CRC) Mhe. Jaji Mstaafu Joseph Warioba, kuhusu uundwaji wa mabaraza katika ngazi ya Kata/Wilaya ina umuhimu wa pekee katika mchakato mzima wa katiba mpya nchini Tanzania. Kwa mantiki hiyo Mtandao wa Jinsia Tanzania inatoa rai na shime kwa Wanawake wote vijijini na mijini kutumia fursa na kujitokeza kwa wingi kujiunga na mabaraza ya Katiba zikiwa zimebaki siku tatu kufikia siku ya mwisho ya kuwasilisha maombi.
Mabaraza ya Katiba ni chombo muhimu, cha kujadili na kuchambua rasimu ya Katiba ambayo itatolewa na Tume ya Katiba mwezi Mei mwaka huu. Hii ni fursa muhimu kwa wananchi hususani wanawake kujadili, kuichambua rasimu na kuhakikisha kuwa imebeba sauti za raia wote na maoni ya makundi yote hususan wanawake na makundi mengine yaliyoko pembezoni.
TGNP tunawakumbusha na kuwaasa wananchi wote hususan wanawake kuchangamkia fursa hii adimu ya kuomba kuteuliwa kuwa miongoni mwa wajumbe wa Baraza katika ngazi ya Kata na Wilaya kama ilivyotangazwa na Tume.
Aina za ushiriki:
• Kutokana na utaratibu uliowekwa, wanawake wote wenye sifa za kuwa wajumbe wanatakiwa kuandika barua kwa Watendaji wa Vijiji/Mitaa kuomba kuteuliwa kujiunga na baraza la Katiba kabla ya muda uliowekwa kumalizika ambao ni Machi 8 hadi 20, 2013.
• Kwa mujibu wa Kifungu kidogo cha (6), Kifungu cha 18 cha Sheria ya mabadiliko ya Katiba, Tume inaweza kuruhusu Asasi, Taasisi au Makundi ya watu kuandaa mikutano kwa ajili ya kutoa fursa kwa wanachama wake kutoa maoni yao juu ya rasimu ya Katiba na kisha kuwasilisha maoni hayo kwa Tume kabla ya August 14, 2013.
Tunatoa wito kwa wanawake wote mmoja mmoja na kwa makundi yenye uwezo kufanya hivyo kulingana na utaratibu huo. Aidha tuwape moyo wenye uwezo miongoni mwetu wajitokeze kwa wingi.
Hata kama tumeshawahi kutoa maoni yetu kwenye mikutano iliyotangulia, bado tunaweza kuomba nafasi hizi, kwa vile hii sasa ni rasimu ya katiba yenyewe, na ushiriki wetu mpana kwenye mabaraza ya kata na wilaya utatuwezesha kujadili na kuichambua kwa umakini zaidi rasimu ya Katiba na kuhakikisha madai yetu tuliyoyawasilisha wakati Tume ilipopita kukusanya maoni yamezingatiwa. Tusisahau kuhakikisha masuala yenye kuzingatia haki za kijamii yameingizwa na kuwa masuala ya kijinsia yamepewa kipaumbele. Tunataka Katiba itakayobeba sauti na maoni yetu ikilinda maslahi ya jamii nzima bila ubaguzi wa aina yeyote. Muda uliotolewa kuwasilisha maombi ni Machi 8 hadi 20, 2013.