‘Tulipanua Elimu kwa Sababu Tulikuwa nyuma’

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali yake iliamua kupanua kwa kiwango kikubwa elimu nchini kwa ngazi zote kwa sababu Tanzania ilikuwa nyuma sana ya nchi nyingine jirani katika sekta ya elimu miaka saba iliyopita.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake ilichukua uamuzi huo wa busara kwa sababu vijana wengi wa Tanzania waliostahili kupata elimu ya awali, msingi, sekondari, ufundi na elimu ya juu walikuwa hawaipati elimu hiyo.

Rais Kikwete ameyasema hayo, Machi 14, 2013, wakati alipo hutubia wanajumuiya ya Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro (MUM) na wananchi wanaoishi jirani na chuo hicho baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye Ujenzi wa Jengo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na kufungua Jengo la Kitivo cha Sayansi kwenye chuo hicho kwenye eneo la Msamvu, mjini Morogoro

Rais Kikwete amewaambia wananchi hao: “Katika Kipindi cha miaka saba, Serikali yetu imeongeza sana uwekezaji katika upanuzi wa elimu tangu ya awali hadi elimu ya juu. Tuliamua kufanya hivyo kwa sababu vijana wengi waliokuwa wanastahili kupata elimu ya awali, msingi, sekondari, ufundi na elimu ya juu walikuwa hawaipati.”

Ameongeza: “Tanzania ni kubwa mara mbili kuliko Kenya na mara tatu kuliko Uganda kwa eneo na idadi ya watu lakini sisi ndiyo tulikuwa na idadi ndogo zaidi ya wanafunzi katika ngazi hizo zote. Kwa mfano, mwaka 2005, idadi ya wanafunzi waliokuwa Chuo Kikuu nchini Kenya ilikuwa 108, 407, Uganda 88,360, na baadhi ya nchi za SADC kama vile Afrika Kusini idadi hiyo ilikuwa 717, 973. Wakati wenzetu walikuwa na idadi hiyo, sisi tulikuwa na wanafunzi 40, 719 tu katika vyuo vikuu nchini.”

Amesisitiza Rais Kikwete: “ Hali hiyo ilikuwa pia kwa elimu ya sekondari. Kenya ilikuwa na wanafunzi 925,341, Uganda 619,519 na Afrika Kusini 4,186,882 wakati Tanzania ilikuwa na wanafunzi 524,325 tu waliokuwa katika shule za sekondari. Hali hii haikukubalika na tukaamua hatuwezi kuiachia iendelee. Tukachukua hatua tulizozichukua.”

Rais Kikwete amesema kuwa matokeo ya uamuzi ni kwamba vijana wengi wa Tanzania leo wanapata fursa kubwa zaidi za elimu kuliko wakati wowote katika “historia ya nchi yetu.” Amesema kuwa sasa kazi inayoendelea ni kuimarisha ubora wa elimu wapatayo vijana wa Tanzania kwa kuongeza idadi ya walimu, vifaa vya kufundishia na vitabu.

Ameongeza Rais Kikwete: “Kufuatia juhudi hizo, idadi ya wanafunzi waliopo kwenye vyuo vikuu nchini imeongezeka sana, kutoka wanafunzi 40,719 mwaka 2005 hadi kufikia 166,484 mwaka 2012. Kwa upande wa sekondari mwaka 2011 tulikuwa na wanafunzi milioni 1.79 na wenzetu wa Kenya walikuwa na wanafunzi 1.77. Haya ni mafanikio makubwa na Serikali itaendelea kuwekeza katika upanuzi wa fursa za elimu na ubora wake.”

Rais Kikwete pia amesifu, kupongeza na kuwashukuru wadau wengine wa elimu ambao wametoa mchango mkubwa katika kupanua fursa ya elimu kwa vijana wa Tanzania. “Kwa mfano, katika vyuo vikuu 49 vilivyopo nchini kwa sasa, vinavyomilikiwa na umma ni 14 tu. Vyuo vikuu 24 vinamilikiwa na mashirika ya dini na 11 ni vya sekta binafsi.”