NA: FRANK SHIJA & BENEDICT LIWENGA- MAELEZO
MWANASIASA mkongwe nchini Mzee Kingunge Ngombale Mwiru amewataka viongozi kukienzi na kuthamini lugha ya Kiswahili ili kuendelea kujenga taifa lenye umoja na mshikamano.
Kauli hiyo ilitolewa na Mzee Kingunge ambaye alikuwa mgeni ramsi katika hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha Historia ya Hayati Sheikh Kaluta Amri Abedi iliyofanyika kwenye ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam .
“Hatima ya Taifa inategemea lugha ya Kiswahili. Viongozi wanawajibu mkubwa katika kuhakikisha kuwa lugha ya Kiswahili inakuwa kwani wao ndio wanaweza kukipandisha au kuiua lugha ya Kiswahili kwakuwa jamii inawategemea kwa kiasi kikubwa,” alisema Mzee Kingunge.
Aidha Mzee Kingunge amewaasa watanzania wote kuwa wazalendo na kutumia lugha yao kwa ufasaha tofauti na ilivyo sasa katika shughuli mbalimbali pia aliunga mkono lugha hiyo kuwa rasmi kufundishia, lakini ametoa changamoto kuwa yatupasa kuwa makini katika kuitumia hususani katika ngazi elimu ya msingi, sekondari hadi vyuo vikuu.
“Kama kufundisha lugha ya Kiswahili katika elimu ya sekondari ni tatizo na Kiingereza ni tatizo . Kiswahili kipi kifundishwe katika elimua ya Chuo Kikuu,”alisema. Huku akitolea mfano kuwa kumekuwa na matumizi ya maneno ambayo si sahihi kama vile neno masaa badala ya saa.
Kwa upande wake mwanazuoni na mdau wa lugha hiyo Profesa Mugyabuso Mulokozi na Profesa Joshua Madumula wameiomba serikali kuwa na utaratibu wa kuenzi fasihi za Watanzania.