Rais Kikwete Ashiriki Msiba wa Yanga

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Katibu Mkuu wa Yanga Lawrence Mwalusako katika mazishi ya mchezaji mkongwe wa Yanga na baadaye Kocha wa Pan Africa Marehemu Athumani Kilambo leo Machi 11, 2013 katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es salaam. wengine toka kushoto ni Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika. Ndugu Adam Malima, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es salaam Mhe Ranmadhani Madabida na kulia ni Mwenyekiti wa Yanga Bw. Yusuf Manji.

Rais Jakaya Kikwete akiondoka baada ya kuongoza maelfu ya waombolezaji katika mazishi ya mchezaji mkongwe wa Yanga na baadaye Kocha wa Pan Africa Marehemu Athumani Kilambo leo Machi 11, 2013 katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam. (PICHA ZOTE NA IKULU).

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatatu, Machi 11, 2013, amejiunga na mamia ya waombolezaji kumzika aliyekuwa mchezaji hodari wa timu ya soka maarufu ya Yanga ya Dar Es Salaam, Athuman Kilambo.

Athuman Kilambo ambaye alifariki dunia usiku za kuamkia leo baada ya kusumbuliwa kwa muda na ugonjwa wa kansa amezikwa kwenye Makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam. Kilambo alikuwa mlinzi hodari wa kushoto wa timu ya Yanga ambayo aliichezea kwenye miaka ya 1960 na 1970. Alikuwa mmoja wa walinzi imara wa kikosi cha klabu hiyo ambacho kilitawala soka ya Tanzania kwa kushinda ubingwa nchini kwa miaka mitano mfululizo hadi mwaka 1973 wakati Simba ilipowavua ubingwa huo.