Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
WANANCHI wa Chwaka wameeleza kufarajika kwao baada ya kukamilika mradi wa maji safi na salama katika kijiji chao na kuondosha tatizo lililokuwa likiwakabili la ukosefu wa huduma hiyo kwa kipindi kisichopungua miaka saba.
Wakisoma risala yao mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein mara baada ya kuuzindua mradi wa maji safi na salama kijijini hapo akiwa katika ziara yake katika Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja. Katika maelezo yao kwenye risala yao waliyoisoma, wananchi wa Chwaka walitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa msaaada mkubwa wa fedha zilizotumika kuunulia mambomba yaliotumika katika kumalizia mradi huo.
Wananchi hao wa Chwaka walieleza kuwa walijitolea kwa hali na mali katika kufanikisa mradi huo na kuweza kuchangia Tsh. Milioni 37 pamoja na nguvu kazi na kuchimba mtaro pamoja na kufukia mabomba kutoka kisimani hadi Chwaka eneo lenye kilomita 7. Wananchi hao wa Chwaka walitoa shukurani kwa wale wote waliochangia katika mradi huo akiwemo Mwakilishi wa Jimbo hilo Issa Haji Gavu aliyechangia Tsh. Milioni 41 zilizotumika kununulia mabomba na pambu ya kusukumia maji.
Aidha, katika risala yao hiyo wananchi wa Chwaka walitumia fursa hiyo kutoa shukurani kutoka kwa wavuvi wa kijiji hicho kwa kuthamini kilio chao cha muda mrefu. Katika kuufanya mradi huo uwe endelevu wananchi hao wa Chwaka waliahidi kuwa wako tayari kushirikiana na Mamlaka ya Maji (ZAWA) katika kutoa day a matumizi ya maji kama ilivyopangwa na serikali.
Sambamba na hayo, wananchi hao wa Chwaka walimuomba Rais kuwa mlezi wa mradi huo ambapo ombi lao hilo lilikubaliwa na Rais pamoja na maombi yao yote waliyoomba ikiwa ni pamoja na ukarabati wa nyumba ya madaktari pamoja na kupatiwa madaktari.
“Sisi wananchi wa Chwaka tunaahidi kuwa tuko tayari kushirikiana na wewe mwenyewe binafsi pamoja na Serikali yetu ya Umoja wa Kitaifa”,alieleza wananchi hao katika risala yao.
Katika hotuba take Rais wa Zanzibar na Mwwnyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliwapongeza wananchi wa Chwaka kwa uvumilivu wao pamoja na kuipongeza Jumuiya ya Maendeleo ya wananchi wa Chwaka na viongozi wao wa Jimbo pamoja na Mamlaka ya Maji Zanzibar kwa juhudi zao katika kuendeleza mradi huo.
Dk. Shein pia, aliipongeza Wizara yake ya Fedha katka jitihada zake za kuhakikisha mradi huo unafanikiwa huku akieleza kuwa miundombinu ya kupata maji ni mingi na inahitaji fedha nyingi na ndio maana Serikali yake ikaamua kuikopa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), kiasi cha Bilioni 67 kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maji nchini.
Aidha, Dk. Shein aliwasisitiza wananchi hao kuyatumia maji kwa umakini zaidi hasa ikizingatiwa kuwa kiwango cha maji kimepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na mabadiliko ya hali ya Tabia nchi. Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imo katika kufanya jitihada ya kuhakikisha tatizo la maji linapungua kwa kiasi kikubwa hapa nchini kwani tatizo la maji si dogo kama linavyofikiriwa.
“Serikali ina jukumu la kuhakikisha wananchi wake wanapata maji safi na salama na ndio maana imedhamiria kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo ya maji Unguja na Pemba kwa kuanzisha miradi mbali mbali”,alisema Dk. Shein.
Nae Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Mhe. Ramadhan Abdalla Shaaban alieelza kuwa utekelezaji wa mradi wa maji safi na salama wa Chwaka ni miongoni mwa jitihada za Serikal ya Mapinduzi Zazibar ambao umegharimu Tsh. Milioni 330 zimetumika katika ujenzi.
Alisema kuwa mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mkubwa unaoitwa Mradi wa maji salama (Safe Water Project) uliogharamiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzbar kwa kushirikiana an wananchi wa Chwaka.
Akitoa taarifa ya kiufundi Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mirza alieleza kuwa harkati za ujenzi wa mradi huo zilianza Maci 29 mwaka jana kwa kuhimba kisima huko Hanyegwamchana na Mei 17 kazi zote za uchimbaji zilikamilikana tarehe 4, Novemba mradi wote ulimalizika ambapo wananchi wapatao 4600 wanafaidika. Dk. Shein ataendelea na ziara yake kesho katika Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja pamoja na kufanya majumuisho ya ziara yake katika Mkoa huo.