KAMPUNI ya Bia ya Serengeti Breweries kupitia mpango wake wa kuisaidia jamii leo imekabidhi rasmi mradi wa maji uliopo katika Hospitali ya Sekou Toure jijini Mwanza. Mradi huo ulikabidhiwa na Mke wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Salma Kikwete, ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika makabidhiano hayo.
Mradi huo wa maji unatarajia kukidhi mahitaji ya watu zaidi ya 160,000 waishio jijini Mwanza na ambao wanatibiwa au kufika hospitalini ya Sekou Toure. Mradi huu kwa kiasi kikubwa utapunguza mfumuko wa magonjwa na vilevile vifo vya watoto na kina mama wajawazito. Mradi huu wa Hospitali ya Sekou Toure unajumuisha kisima , pampu ya maji ya umeme na tanki la kuhifadhia maji la lita elfu kumi.
Kampuni ya Bia ya Serengeti imetumia kiasi cha shilingi milioni 70 kukamilisha mradi huu. Kisima hiki kina uwezo wa kutoa lita 240,000 kwa siku.
Akiongea katika hafla ya makabidhiano hospitalini Sekou Toure , Mama Salma alisema “ Nafarijika sana kujua kwamba Hospitali hii sasa imepata suluhisho la tatizo la maji walilokuwa nalo hapo awali.Na napenda kuwashukuru sana Kampuni ya Bia ya Serengeti kwa juhudi zao katika kusaidia shughuli za kijamii na hasa katika upatikanaji wa maji safi na salama na hasa katika hospitali zetu.”
Kampuni ya Bia ya Serengeti wamekuwa mstari wa mbele katika kusaidia upatikanaji wa maji safi na salama na tayari wamewezesha miradi mbalimbali ya maji katika maeneo mbalimbali hapa nchini kama vile Iringa – Hospitali ya Frelimo, Moshi – Hospitali ya Mawenzi , Dar-es salaam – Hospitali ya Temeke na ule wa Mkuranga.
Mkurugenzi wa Mahusiano na Mawasiliano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti , Bwana Evans Mlelwa , amesema “Suala la kuisaidia jamii kwa Kampuni ya Bia ya Serengeti limepewa kipaumbele na uzito wa hali ya juu na hasa katika kusaidia upatikanaji wa maji safi , salama na pia endelevu.
Kama Kampuni SBL inatambua umuhimu wa maji kwa binadamu na pia mchango wa maji katika maendeleo ya nchi , kiuchumi na kijamii.Kama Kampuni kutafuta na kupata suluhisho la kudumu ni katika kuhakikisha tunatoa msaada kwa jamii inayotuzunguka na tunakofanya uzalishaji”. Aliongeza Mlelwa “Kampuni ya Bia ya Serengeti na EABL Foundation mpaka sasa tumeshawekeza zaidi ya milioni 300 za kitanzania , katika maeneo mbalimbali ambapo zaidi ya watu 450,000 wanafaidika na miradi hiyo”.