Kampuni Yamuahidi Dk Shein Kukarabati Uwanja wa Ndege kwa Wakati

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK. Ali Mohamed Shein, (katikati) akipata maelezo kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Miundombinu, Dk.Juma Malik
Akili, (kushoto) alipotembelea maendeleo ya Ujenzi wa Uwanja wa Ndege, unaoendelea, akiwa katika ziara ya Wilaya ya Magharibi Unguja iliyomalizika. [Picha na Ramadhan Othman, Ikulu]

KAMPUNI ya Sogea Satom ya Ufaransa imeahidi kukamilisha Mradi wa ukarabati na ujenzi wa njia za kupitia ndege wakati wa kuruka na sehemu ya maengesho ya ndege katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kwa wakati uliopangwa.

Akitoa maelezo kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Meneja Mkuu wa Mradi huo Bwana Sarpone Roberto, alimueleza Dk. Shein kuwa Kampuni yake itahakikisha inafanya kazi hiyo kwa umakini zaidi sanjari na kuutekeleza kwa muda uliowekwa.

Alimeleza kuwa licha ya baadhi ya changamoto ziliopo lakini Kampuni yake itafanya juhudi ya kukamilisha mradi huo ikiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa uzio katika eneo hilo la uwanja wa ndege wa Zanzibar.

Hayo, yalifahamika katika ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ambayo inaendelea katika mikoa yote ya Unguja na Pemba ambapo alipata fursa ya kutembelea ujenzi wa mradi huo unaoendelea.

Mapema uongozi wa uwanja huo ulitoa taarifa ya mradi huo ambazo zilieleza kuwa lengo na madhumuni ilikuwa mradi huo uanze rasmi mnamo tarehe 2.07.2012 lakini kutokana na changamoto mbali mbali ulianza tarehe 20.08.2012.

Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa miongoni mwa changamoto zilizojitokeza ni pamoja na fidia katika eneo la njia za kupitia ndege wakati wa kuruka na sehemu ya maegesho ya ndege.

Pamoja na hayo, ilifahamika kuwa jumla ya Tsh. Bilioni 1.2 kwa ajili ya kuwalipa wananchi waliokuwa wakitumia eneo la mradi kama makaazi na mashamba yao pamoja na fidia kwa ajili ya kuhamisha makaburi 21 yaliokuwemo katika eneo hilo la mradi.

Kutokana na changamoto hizo ilibidi Mkandarasi abadilishe program yake ya kazi na kuanzia kazi katika eneo la njia za kupitia ndege wakati wa kuruka badala ya sehemu ya maegesho ya ndege kama ambavyo alikuwa amepangiwa mwanzoni mwa mradi na wakati wa kuomba kazi hiyo.

Kwa maelezo ya uongozi huo, Mradi huo unatekelezwa bila ya kuathiri urukaji na utuaji wa ndege na bila kuathiri mazingira ya uwanja wa ndege.

Kwa hivi sasa Mkandarasi anaendelea na kazi mbali mbali katika mradi huo ikiwa ni pamoja na kuandaa na kusafirisha kokoto laini ambazo zinachanganywa na changarawe na hatimae hutumika kama tabaka la chini, shughuli zinazofanywa huko katika eneo la Dunga na Kibele Unguja.

Shughuli nyengine zinazofanywa katika mradi huo ni pamoja na kuandaa usafirishaji kokoto ngumu kutoka eneo la Tembo Lugoba Chalinze Dar-es-Salaam hadi Zanzibar ikiwa ni pamoja na kazi za ujenzi wa njia za kupitia ndege wakati wa kuruka.

Na kwa upande wa maegesho ya ndege hivi sasa kazi inaendelea na mkandarasi anamalizia kusafisha eneo lote pamoja na kujaza mashimo mawili makubwa yenye ujazo wa zaidi ya mita za mraba 70,000 ambayo yalitumika kama sehemu ya kuchukulia moramu mnamo miaka ya 70 hadi 80.

Katika ziara yake, hiyo Dk. Shein alitembelea katika eneo hilo la mradi na kuona shughuli hizo za ujenzi zinavyoendelea huku akipata maelezo kutoka kwa uongozi wa Wizara husika pamoja na uongozi wa Kampuni ya Sogea Satom ya Ufaransa.

Mradi huo unafadhiliwa na Benki ya Dunia pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambapo Mradi huo utafanyika kwa muda wa miezi 18 na utagharimu zaidi ya Tsh. Bilioni 65.

Nae Dk. Shein alitoa pongezi kwa hatua hizo za ujenzi zinazoendelea huku akisisitiza haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja katika kuukamilisha na kuutekeleza mradi huo muhimu na mkubwa katika kuimarisha maendeleo na kukuza uchumi wa Zanzibar.