Daktari Mwanza Aeleza Kinachowauwa Wajawazito Wengi

Mjamzito


Na Anna Nkinda – Maelezo, Mwanza

IMEELEZWA kuwa kutokana na tatizo la baadhi ya wajawazito kuchelewa kufika Hospitali mapema kujifungua wengi wao wanakufa kutokana na tatizo la kupasuka kwa mfuko wa uzazi, kutokwa na damu nyingi kabla na baada ya kujifungua na kifafa cha mimba.

Hayo yamesemwa jana na Daktari wa Mkoa wa Mwanza Dk. Valentino Bangi wakati akisoma taarifa ya Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mwanza – Sekou Toure kwa Mke wa Rais Mama Salma Kikwete aliyefika Hospitalini hapo kwa ajili ya kufungua mradi wa kisima cha maji uliojengwa na Kampuni ya bia ya Serengeti.

Dk. Bangi alisema kuwa tatizo la vifo vya kina mama wajawazito na watoto limepungua kwa kiasi kikubwa katika Hospitali hiyo ukilinganisha na miaka ya nyuma kwani mwaka 2012 vifo vilivyotokana na tatizo la uzazi vilikuwa 10 ukilinganisha na mwaka 2011 ambapo kulikuwa na vifo 15.

“Kiwango cha utoaji wa chanjo kwa watoto kimeongezeka katika mkoa wetu na kufikia asilimia 95, jumla ya watoto 91194 ambao ni sawa na asilimia 85 waliolazwa walipata chanjo ya pepopunda na vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja ni vimepungua na kufikia 11 kati ya vizazi hai 1000”, alisema Dk. Bangi.

Aliendelea kusema kuwa wamefanikiwa kukarabati jengo la upasuaji, wodi ya watoto, wagonjwa mahututi wodi ya kujifungua kina mama, kuajiri watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo madaktari bingwa watano, ujenzi wa vyumba vya kuhifadhia chanjo, jengo la wagonjwa wa afya ya akili, na maabara ya kisasa kupitia msaada wa watu wa Marekani.

Dk. Bangi alizitaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni upungufu wa dawa, vifaa tiba na watumishi wenye ujuzi, bajeti finyu katika uendeshaji wa huduma za afya, uchakavu wa majengo, kukosa mfumo imara wa rufaa kuanzia zahanati hadi hospitali ya rufaa, ukosefu wa nyumba za watumishi, kushindwa kukamilisha jengo la upasuajai la akina mama wajawazito na kuongezeka kwa makundi mbalimbali ya misamaha katika kutoa huduma za afya.

Kwa upande wake Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliishukuru kampuni ya bia ya Serengeti kwa kujenga mradi wa kisima cha maji ambacho kitapunguza tatizo la maji katika Hospitali hiyo na kusema kuwa kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele kutoa michango ya maendeleo na hasa kusaidia miradi ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa jamii ambayo imeonyesha tija na kuboresha maisha ya watanzani kwa kujenga jamii yenye afya bora kwa maendeleo kwa taifa.

Mama Kikwete alisema, “Maji ni nguzo kubwa kwa maendeleo katika nyanja zote za kiuchumi na kijamii mahali popote pale Duniani, hakika kukamilika kwa mradi huu ni hatua muhimu sana ya kuboresha huduma za maji katika hospitali zetu hapa nchini, ambazo zinahitaji huduma ya uhakika ya maji safi na salama ili kukidhi mahitaji mbalimbali ya wagonjwa pamoja na ya watoa huduma”.

Alimalizia kwa kutoa wito kwa uongozi wa Hospitali hiyo kuulinda mradi wa maji ili kuufanya uwe endelevu, kwa kufanya hivyo mradi huo utakuwa umetoa mchango mkubwa katika kuendeleza ufanisi wa huduma kwa wagonjwa na wataalamu wa afya.

Akisoma taarifa ya mradi huo Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa kampuni ya bia ya Serengeti Jaji Mark Bomani alisema kuwa mradi wa maji umegharimu zaidi ya sh. milioni 70 na una kisima kinachoweza kutoa lita 240,000 za maji kwa siku, pampu ya maji ya umeme na tanki la lita 10,000.

“Kampuni yetu kupitia mpango wake wa kuisaidia jamii na mpango rasmi wa kusaidia upatikanaji wa maji safi na salama leo imefikia lengo la kusaidia watu zaidi ya 160,000 wanaohudumiwa na Hospitali hii, hakika mradi huu utachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza magonjwa ya mlipuko na vifo vya kina mama wajawazito na watoto”, Jali Bomani alisema.

Alisema kuwa kwa kutambua umuhimu wa kuisaidia jamii na siyo tu kupitia miradi ya maendeleo bali pia kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakuwa endelevu na kuleta tija kwa jamii husika. Kampuni hiyo pia wanaisaidia jamii katika upande wa afya, mazingira na kutoa ufadhili wa masomo wa elimu ya juu kwa wanafunzi ambao wamefanya vizuri lakini hawana uwezo wa kumudu gharama za masomo.

Licha ya kujenga maradi wa kisima cha maji katika hospitli hiyo, kampuni hiyo pia imeshafadhili miradi mingine ya maji ambayo imewafikia watu 350,000 katika Hositali za Frelimo-Iringa, Temeke – Dar es Salaam, Mawenzi – Moshi na mradi wa maji wa mkuranga ambao unawahudumia watu zaidi ya 250,000.