Na dev.kisakuzi.com
MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mtanzania amevamiwa na watu wasiojulikana jana usiku nyumbani kwake maeneo ya Mbezi jijini Dar es Salaam na kukatwa mapanga na kupigwa na nondo hali iliyomsababishia majeraha makubwa.
Kibanda ambaye kwa sasa amelazwa katika Kitengo cha Taasisi ya Mifupa, Moi alikuwa na hali hiyo jana majira ya saa saba za usiku alipokuwa akirejea nyumbani kutokea ofisini kwake. Akizungumza na dev.kisakuzi.com mmoja wa wahariri wa Gazeti la Mtanzani, Mareges Paul amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo amesema Kibanda kwa sasa amelazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), Moi.
Alisema kwa mujibu wa taarifa walizozipata kiongozi huyo Mkuu wa Wanahabari Tanzania alivamia na watu wasiojulikana wakiwa na silaha za jadi kama mapanga na nondo akiwa nje ya geti la nyumba yake na kuanza kupigwa na kundi hilo la watu kisha kumtoa kwenye gari lake na kuendelea kumpiga hadi alipotokea mlinzi wa nyumba yake na kuomba msaada kwa majirani.
Alisema watu hao wanaosadikiwa kuwa majambazi wamemcharanga mapanga, kumpiga kwa kutumia vipisi vya nondo na kumtoboa jicho la kushoto, kumng’oa kucha na jino tukio ambalo lilimuacha katika hali mbaya baada ya wavamizi kukimbia. “Ameumia vibaya kwa kweli maana wamemkata mapanga, kumpiga na nondo, kumtoboa jicho la kushoto…,” alisema Paul akizungumzia tukio hilo.
Hata hivyo amesema tayari taratibu zinafanywa kumsafirisha Kibanda kuelekea Afrika Kusini kwa matibabu zaidi. Zaidi endelea kufuatilia mtandao wa www.thehabari.com.