MAKAMU wa Rais wa Venezuela Nicholas Marduro ametangaza kifo cha Rais Hugo Chavez (58) kufuatia kuugua kwa muda mrefu maradhi ya Saratani. Rais Chavez alikuwa katika matibabu nje ya nchi yake kwa muda mrefu ambapo alikuwa akipatiwa matibabu yake nchi Cuba.
Alirejea , mjini Caracas mnamo Februari 18 kwa mara ya kwanza tangu maradhi yake yazidi kumsumbua na kupelekwa hospitali ya kijeshi kuendelea kupata matibau. Hata hivyo maelezo zaidi hayakutolewa juu ya afya yake. Waandamanaji waliandamana katika Mji Mkuu Caracas mwishoni mwa juma wakidai kuwa watu wa Venezuela wanapaswa kupewa habari zaidi kuhusu afya ya rais wao.
Taarifa zinasema Chavez amekua uongozini nchini Venezuela kwa miaka 14 na anatazamiwa kuleta mageuzi makubwa yaliyolenga zaidi kuimarisha maisha ya raia wa pato la chini. Ujumbe wa Jeshi umesema utaendelea kuilinda hadhi ya nchi na kuimarisha usalama. Pia jeshi limeahidi kuendelea kuwa waaminifu kwa makamu wa rais Nicholas Marduro na wakatoa wito kwa raia kuwa watulivu.
Hugo Chavez alijitosa katika siasa za Venezuela mnamo Februari 1992 akiwa luteni katika jeshi. Aliongoza mapinduzi dhidi ya rais wa wakati huo Carlos Andres Perez. Lakini kutokana na kukosa usaidizi wa kutosha wa kijeshi, Chavez na wanamgambo wenzake walishindwa kunyakua madaraka hayo. Alikiri kushindwa na aliwekwa korokoroni.
Aliingia uongozini baada ya ushindi mkubwa ulioviondosha vyama vya kisiasa wakati huo. Katika kuapishwa kwake mnamo February 1999, Hugo Chavez alitangaza wazi kwamba mipango yake ya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi sio kampeni tu. Alitimiza ahadi yake na kuiongoza nchi hiyo katika mabadiliko ambayo hayakuwahi kushuhudiwa katika muda wa miongo kadhaa. Alibadili muundo wa bunge na kulifanya kuwa la kikatiba, ambalo liliiunda katiba mpya baada ya kura ya maoni iliyoidhinishwa na 88% ya wapiga kura.
Rais Chavez alitaifisha rasilmali ukiwemo utajiri wake mkubwa wa mafuta. Sera kama hizi zilimfanya azozane na kampuni za kimataifa za mafuta, lakini alipata uungwaji mkono mkubwa wa watu maskini. Kutokana na urafiki wake na viongozi wa mrengo wa kushoto kama vile rais wa Cuba, Fidel Castro, ambaye walikuwa na uhusiano wa karibu aligongana kidiplomasia na Marekani, ambayo ni mshirika wake mkuu wa kibiashara.
Chavez alipendwa nyumbani na wafuasi wake lakini alipingwa na baadhi ya watu nchini humo na katika nchi za nje. Alionekana sio tu kama bingwa wa jamii maskini lakini pia kama muingiliaji wa siasa za nchi jirani. Katika miaka ya hivi karibuni alilenga kukabiliana na masuala ya ndani ya Venezuela, kama uhalifu, kuinua uchumi wa nchi na kukabiliana na rushwa.
-BBC