Wanawake wanaotafuta ‘weupe’ kuangamia-TFDA

Baadhi ya wananchi wakipata maelezo kutoka katika banda la TFDA linaloshiriki katika maadhimisho ya Wiki wa Utumishi wa Umma Dar es Salaam.

Na Anicetus Mwesa
MAMLAKA ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imesema maelfu ya Watanzania huenda wakaangamia kwa ugonjwa hatari wa Kansa. Imebainishwa kwamba watakaoangamia ni wale wanaotumia vipodozi feki kwa lengo la kutaka kujichubua wawe weupe, ambavyo vina viambata sumu.
Hayo yamebainishwa jana na Mkaguzi wa Dawa na Vipodozi wa TFDA, Kissa Mwamwitwa Dar es Salaaam katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja.
Alisema siyo kila kipodozi kina kidhi haja kwa mtumiaji bali vingi ni feki na kwamba vina madhara makubwa kwa watumiaji yakiwamo magonjwa kadhaa.
“Watu wanaotumia vipodozi visivyo na sifa hasa, wanawake na hata wanaume wanaojichubuwa ili wawe weupe wako hatarini kukumbwa na ugonjwa wa kansa na madhara mengine…, tunawashauri wasikimbilie kila kipodozi wanachoona huko mitaani bila kuvisoma ama kuangalia kama vipodozi hivyo vinafaa ama ni feki,” alisema Mwamwitwa.
Ofisa Habari na Muelimishi Umma wa mamlaka hiyo, Martini Malima alisema TFDA imeimarisha mifumo ya udhibiti wa ubora na usalama wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba ila bado inakabiliwa na changamoto kadhaa.
Malima alisema changamoto hizo ni pamoja na Tanzania kuwa na mipaka mingi hivyo kufanya kazi ya kuwadhibiti wafanyabiashara wanaoingiza madawa feki kuwa ngumu.
“Kuna mipaka takriban 31 ya kuingilia nchini, hivyo mamlaka kama mamlaka kuweza kudhibiti njia zote hizo na zile za panya ni kazi ngumu kidogo. Hivyo ili kuweza kumaliza tatizo hilo ni tunawaomba wananchi watusaidie kutoa taarifa wakiona bidhaa feki.
…Wananchi ndiyo watumiaji na waathirika wa madawa hayo hivyo tunawaomba wasikae kimya iwapo watabaini dawa ama vipodozi visivyo na sifa ama muda wake umeisha watufahamishe na sisi tutachukua hatua dhidi ya muhusika,” alisema Malima.