Kinana Amlilia Waziri wa EAC wa Uganda

Abdulrahman Kinana


Na Mark Mugisha,EANA
SPIKA wa zamani wa Bunge la Afrika Mashariki na Mkuu wa Ujumbe wa Waangalizi wa EAC katika Uchaguzi nchini Kenya, Abdulrahman Kinana amemwelezea Eriya Kategaya aliefariki mwishoni mwa wiki kuwa ni mwenye msimamo na aliyesimamia kikamilifu misingi ya mtangamano EAC.

Kategaya alizaliwa mwaka 1945 Magharibi ya wilaya Ntungamo nchini Uganda na alikufa Jumamosi iliyopita jijini Nairobi alikokuwa amelazwa kwa matibabu, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) linaripoti.

“Tumempoteza mzalendo wa kweli wa Afrika Mashariki.Alikuwa mpole lakini makini katika masuala ya msingi,” Kinana alisema.

Kabla ya kifo chake, Kategaya ambaye alikuwa ni rafiki wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda tangu utotoni, alikuwa Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariiki na anakumbukwa kuwa mhimili mkuu wa kusukuma mbele mtangamano wa EAC kwa haraka. Waziri wa EAC wa Rwanda, Monique Mukaruliza alisema kanda ya EAC itamkosa sana Naibu huyo wa Tatu wa Waziri Mkuu wa Uganda na Waziri wa EAC kwa miongozo yake ya busara katika masuala mbalimbali ya EAC.

“Temepoteza hazina kubwa katika jumuiya na tutakuwa tunakosa kila mara uzoefu wake mkubwa na mchango wake katika mikutano mbalimbali ya EAC,” Mkaruliza alisema.

“Rambirambi zetu ziwafikia familia,ndugu na serikali ya Uganda kufuatia taarifa hii ya kuhuzunisha ya kifo cha Mheshimiwa Kategaya,” alisema Waziri huyo wa Rwanda.

Kihistoria Kategaya alikuwa ni mwanachama wa chama tawala nchini Uganda cha RNM, ambaye kwa miongo kadhaa alikuwa anafanyakazi bila kuchoka kuikomboa Uganda. Straton Ndikuryayo, Mbunge wa Rwanda katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) alisema Kategaya alikuwa makini kuhakikisha kwamba wanaafrika Mashariki wanachangia ipasavyo juu ya mtangamano wao wa EAC.