Pinda Azindua Tume, Aitaka Itafute Muarobaini wa Kushuka kwa Elimu

Bw. Rakhesh Rajani mdau wa elimu kutoka TWAWEZA


*Ni ya watu 15, aipa wiki sita kukamilisha kazi
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amezindua Tume maalum aliyoiunda kuchunguza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yaliyotangazwa Februari 18, mwaka huu na kuwataka wajumbe wa Tume hiyo watafute kiini cha kushuka kwa kiwango cha ufaulu kuanzia mwaka 2010 hadi 2012.

Ametoa kauli hiyo Machi 2, 2013 wakati akizungumza na wajumbe wa Tume hiyo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni, jijini Dar es Salaam. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.

“Nimetafuta takwimu za tangu mwaka 2005, Serikali ya Awamu ya Nne ilipoingia madarakani na kubaini kuwa tangu wakati huo hadi mwaka 2009 tulikuwa tukifanya vizuri, lakini kuanzia mwaka 2010 hadi 2012 matokeo yamekuwa yakishuka sana,” aliwaambia wajumbe wa Tume hiyo na waandishi wa habari waliohudhuria uzinduzi huo.

Alisema hali hiyo haikuwa kwenye shule za sekondari za umma (kata) peke yake bali hata kwa shule za Serikali, za watu binafsi na kwenye seminari ambazo kwa miaka mingi zimekuwa na sifa ya kufanya vizuri kuliko shule za kawaida.

Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema: “Mwaka 2005 kiwango cha ufaulu kilikuwa asilimia 89.3; mwaka 2006 asilimia 89.12; mwaka 2007 asilimia 90.6; mwaka 2008 asilimia 83.6 na mwaka 2009 asimilia 72.5, hapa napo tulikuwa bado tuko vizuri japo si sana ikilinganishwa na miaka mine iliyotangulia.”

“Lakini mwaka 2010, kiwango cha ufaulu kilishuka na kufikia asilimia 50.4, mwaka 2011 kilipanda kidogo na kufikia asilimia 53.6 na kilishuka zaidi mwaka jana ambapo kilifikia asilimia 34.5. Hapa ni lazima mtu utapata maswali ya msingi na kujiuliza nini kimetokea katika miaka ya hivi karibuni,” alisema.

Waziri Mkuu alibainisha kwamba idadi ya watahiniwa iliongezeka kutoka 85,292 mwaka 2005 na kufikia 248,336 katika mwaka 2009 wakati idadi ya walimu nayo pia iliongezeka kutoka 20,414 na kufikia 37,218 katika kipindi hichohicho.

Alisema anatambua changamoto nyingine zinazoikabili sekta ya elimu kama vile uhaba wa vitendea kazi, upungufu wa maabara na walimu wa sayansi, upungufu wa mabweni pamoja na nyumba za walimu. Kinachoshangaza, Waziri Mkuu alisema, mbali na kuongezeka kwa walimu kutoka 44,053 mwaka 2010, walimu 55,982 (mwaka 2011) na kufikia walimu 68,784 mwaka 2012 bado kiwango cha ufaulu nacho kilikuwa kikishuka katika kipindi hichohicho.

Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema: “Kwenye shule za kata, mwaka 2010, walifaulu wanafunzi 114,883; mwaka 2011 wanafunzi 106,286 na mwaka 2012 wanafunzi 74,817 wakati kwenye shule za Serikali, katika kipindi hicho hicho ufaulu ulishuka kutoka wanafunzi 19,412, na kufikia wanafunzi 10,712.”

Waziri Mkuu alisema katika mchanganuo huo, jambo moja kuu lililo bayana ni kuwepo kwa mzao wa kwanza wa shule za kata katika mwaka 2010 lakini bado athari za kushuka kwa ufaulu zikasambaa kote hadi kwenye shule za serikali, za binafsi na seminari. Akianisha kushuka kwa ufaulu wa daraja la kwanza katika makundi hayo, Waziri Mkuu alisema: “Mwaka 2010, kwenye shule za kata, walifaulu wanafunzi 1,225 wakati mwaka 2011 walikuwa wanafunzi 564 na mwaka 2012 walikuwa wanafunzi 162”.

“Kwenye shule za Serikali, mwaka 2010, walifaulu wanafunzi 952, mwaka 2011 wanafunzi 771 na mwaka 2012 wanafunzi 253. Kwenye shule za binafsi, mwaka 2010, walifaulu wanafunzi 2,476 mwaka 2011 wanafunzi 1,614 na mwaka 2012 wanafunzi 1,032. Kwenye seminari, mwaka 2010, walifaulu wanafunzi 695, mwaka 2011 wanafunzi 428 na mwaka 2012 wanafunzi 197.”

Akianisha matokeo ya waliofeli kwa kupata daraja ‘0’, Waziri Mkuu alisema: “Mwaka 2010, kwenye shule za kata, walifeli wanafunzi 151,848 wakati mwaka 2011 walifeli wanafunzi 143,552 na mwaka 2012 walifeli wanafunzi 223,774”.

“Kwenye shule za Serikali, mwaka 2010, walifeli wanafunzi 7,926, mwaka 2011 wanafunzi 9,790 na mwaka 2012 wanafunzi 16,176. Kwenye shule za binafsi, mwaka 2010, walifeli wanafunzi 13,346 mwaka 2011 wanafunzi 16,620 na mwaka 2012 wanafunzi 25,055. Kwenye seminari, mwaka 2010, walifeli wanafunzi 638, mwaka 2011 wanafunzi 972 na mwaka 2012 wanafunzi 1,329.”

Alisema kwa mujibu wa hadidu za rejea, wajumbe wa tume hiyo watatakiwa kuangalia ni sababu zipi zimechangia kuwepo kwa matokeo hayo mabaya, mserereko wa kushuka umekuwa ukiongezeka kwa sababu gani, usimamizi katika Halmashauri ukoje, ukaguzi wa elimu na uhamishiwaji wa sekta ya elimu kwenye Wizara ya TAMISEMi umechangiaje kushuka kwa kiwango cha ufaulu.

Vilevile, watatakiwa kuangalia mitaala na mihutasari ikoje, kuangalia uwiano uliopo kwenye mitihani inayotungwa ikiwa ni pamoja na uhakiki wa mitihani hiyo; kuangalia mazingira ya kufundishia, mfumo wa upimaji, usimamizi na uendeshaji, na kutokuwepo kwa chakula shuleni kunachangiaje kushuka kwa utendaji mbaya wa wanafunzi katika masomo yao.

Tume hiyo yenye wajumbe 15, imepewa muda wa wiki sita kuanzia Machi mosi iwe imekamilisha kazi hiyo na kuwasilisha taarifa yao kwa Waziri Mkuu. Itaongozwa na Prof. Sifuni Mchome wa Tume ya Vyuo Vikuu, na Makamu wake atakuwa Bi. Bernadetha Mushashu (Mbunge wa Viti Maalum – Kagera).

Wajumbe wengine ni Bw. James Mbatia (mbunge wa Kuteuliwa), Bw. Abdul J. Marombwa (Mbunge wa Kibiti), Prof. Mwajabu Possi (Chuo Kikuu – UDSM), Bibi Honoratha Chitanda (CWT) na Bibi Daina Matemu (TAHOSSA) na Bw. Mahmoud Mringo (TAMONGSCO).

Wengine ni Bw. Rakhesh Rajani (TWAWEZA), Bw. Peter Maduki (CSSC), Mwl. Nurdin Mohamed (BAKWATA), Bw. Suleiman Hemed Khamis (Baraza la Wawakilishi), Bw. Abdalla Hemed Mohamed (Chuo Kikuu – SUZA), Bw. Mabrouk Jabu Makame (Baraza la Elimu Z’bar na Bw. Kizito Lawa (Taasisi ya Kukuza Mitaala)