Na Isaac Mwangi, EANA
MWENYEKITI wa Tume ya Uchaguzi Kenya (IEBC), Ahmed Isaack Hassan ametoa wito kwa vyama vya siasa kuheshimu matokeo ya uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika mapema wiki ijayo.
Hassan alisema hayo alipokuwa anawapokea wakuu wa wajumbe wa Timu za Uangalizi wa Uchaguzi huo kutoka Taasisi Tatu za Kiuchumi za Kanda( RECs) waliomtembelea ofisni kwakeJumatano. Walifuatana na afisa mwandamizi wa IECB, James Oswago, Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) limeripoti.
Ujumbe huo unajumuisha Abdulrahman Kinana, Mkuu wa Timu ya Waangalizi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Berhane Ghebray, Mkuu wa Timu ya Mamlaka ya Maendeleo ya Afrika na Mkuu wa Soko la Pamoja la Nchi za Kusini mwa Afrika, Simbi Veke Mubako.
Makundi hayo yote matatu yana jumla ya waangalizi wa uchaguzi 78. Wanashrikiana katika kuwaweka maeneo mbalimbali waangalizi wao wa uchaguzi ili kuongeza wigo wao katika kutathmini uchaguzi huo hapo baadaye.
Hassan aliwakumbusha wagombea ahadi walizotoa walipokuwa wanatia saini makubalino ya uendeshaji wa uchaguzi. Aliwataka kuendesha shughuli zao kwa amani bila kushutumiana. Kama hawatakubaliana na matokeo basi alisema wapeleka malalamiko yao mahakamani.
Mkuu wa Tume hiyo alionyesha kujiamini kwamba tume yake ina uwezo wa kushughulikia masuala ya kura kwa kusema waliweza kusimamia vizuri kura za maoni ya Katiba Mpya mwaka 2010, uchaguzi wa Bunge katika majimbo 16 na uchaguzi wa serikali za mitaa katika maeneo zaidi ya 60.
Kwa niaba ya ujumbe huo, Kinana, Mkuu wa Ujumbe wa EAC, alisema Timu ya Waangalizi imeridhishwa na hatua ilizochukua kuhakikisha kuwa unachaguzi huo unafanyika katika hali huru na haki. Machi 5, timu hiyo ya pamoja ya RECs itakutana mjini Nairobi ambako itatoa tathmini yao ya awali juu ya uchaguzi huo.