Mama Salma Kikwete Asisitiza kliniki kwa Wajawazito

Mama Salma Kikwete-WAMA


Na Anna Nkinda – Maelezo, aliyekuwa Sumbawanga

WAJAWAZITO wametakiwa kuhudhuria kliniki mapema pale wanapojitambua kuwa na ujauzito hii itawasaidia kupata huduma mbalimbali za afya ikiwa ni pamoja na kupima afya zao na kuona kama wanambaambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) au la na hivyo kujifungua salama mtoto asiye na maambukizi ya ugonjwa huo.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alipokuwa akiongea na wananchi wa wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa wakati akikabidhi pikipiki 10 za programu ya kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) zilizotolewa kwa ufadhili wa Walter Reed HIV/AIDS Program.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa afya wanahangaika kuhakikisha kuwa watoto watakaozaliwa hawana maambukizi ya VVU kwani dawa za kuzuia maambukizi zipo ni jukumu la kina mama kuhudhuria kliniki mapema na kupima afya zao.

“Janga la Ukimwi ni tatizo kubwa kwa jamii yetu. Natoa Rai kwa wananchi wote tuwe waangalifu kujikinga na ugonjwa huu. Kutokana na takwimu zinaonyesha kuwa hali ya maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) kwa Mkoa huu ni 5.6% hivyo basi uwepo wa baba unatakiwa ili kuboresha afya ya mama na mtoto”, alisema Mama Kikwete.

Mwenyekiti huyo wa WAMA pia aliwaasa wote waliokabidhiwa pikipiki hizo kuzitunza na kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa. Na kuwakumbusha kuwa pikipiki hizo ni kwa ajili ya ukusanyaji wa sampuli za damu kutoka vituo vilivyo mbali zaidi na wilaya na kuvipeleka kwenye Maabara ya Kanda na pia kuimarisha mawasiliano kati ya kituo na kituo na si vinginevyo.

Akisoma taarifa ya mradi huo Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi Mkoa wa Rukwa Dk. Shadrack Mtulla alisema kuwa wana vituo vya kutolea huduma za afya 267 kati ya hivyo 177 vinatoa huduma PMTCT ambavyo ni sawa na asilimia 66 ya vituo vyote na kipindi cha mwaka 2012 jumla ya akina mama 3189 waliandikishwa katika vituo vya kutolea huduma na malezi yaani CTC na kupewa dawa za ARV.

Alisema kuwa, kwa kushirikiana na Walter Reed HIV/AIDS Program katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi kwa kipindi cha mwaka 2012/2013 wamenunua pikipiki 10 ambazo zitagawanywa katika vituo vya afya ambavyo viko mbali na makao makuu ya wilaya katika wilaya zote za mkoa huu.

Dk. Shadrack Mtulla alisema, “Upatikanaji wa pikipiki hizi utarahisisha ukusanyaji wa sampuli za damu kutoka vituo vilivyopo mbali zaidi na wilaya, na kuzileta katika maabara tayari kwa kuzisafirisha kwenda katika maabara za kanda pia zitaboresha mawasiliano kati ya kituo na kituo na hivyo kurahisisha ukusanyaji wa takwimu kutoka vituo mbalimbali kwa muda uliopangwa”, Dk. Shadrack Mtulla.

Dk. huyo alizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni upungufu mkubwa wa vyombo vya usafiri hususani magari kwani mkoa huo una magari mawili na mahitaji halisi ni sita, upungufu wa wataalamu wa afya vituoni, watumishi walioko katika vituo vya kutolea huduma ni asilimia 35 na upatikanaji wa vitendanishi usiokidhi mahitaji ya mkoa na wilaya zake.

Pikipiki hizo zilikabidhiwa kwa wakurugenzi wa halmashauri za wilaya ya Sumbawanga tatu kwa ajili ya vituo vya Afya vya Milepa, Kasanga na Mwitu, Nkasi mbili kwa ajili ya vituo vya afya Kirando na Kilangalanga, Manispaa ya Sumbawanga mbili ambazo zitatumika katika vituo vya afya vya Ntembo na Ulinji, Mji wa Mpanda moja kwa ajili ya kituo cha Afya Mwangaza na wilaya ya Mpanda ambazo zitatumika katika vituo vya afya Mamba na Mishano.