Dk Shein Ajivunia Jitihada za SMZ Kuinua Uchumi wa Wazanzibari

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akimkabidhi zawadi ya Mlango wa
Zanzibar, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Yussuf bin Alawi Bin Abdullah, alipofika Ikulu Mjini Zanzibar akiwa na Ujumbe wake (Picha na Ramadhan Othman, IKulu)



Na Said Ameir, Ikulu Zanzibar

JITIHADA za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa katika kipindi chake cha miaka miwili ya mwanzo zimejenga mwelekeo na mwenendo mzuri katika kuimarisha uchumi na ustawi wa wananchi katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati wa mazungumzo na Waziri wa anayesimamia masuala ya Mambo ya Nje wa Oman Bwana Yousuf bin Alawi bin Abdullah.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu leo Dk. Shein amesema mwelekeo huo mzuri umeonekana katika nyanja mbalimbali kwa mfano kupunguza mfumuko wa bei na kukua kwa uchumi kutoka asilimia 6.5 mwaka 2010 hadi asilimia 7 mwishoni mwa mwaka 2012.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza na Ujumbe wa Serikali ya
Watu wa Oman, ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Yussuf bin Alawi Bin Abdullah, (wa pili kulia) alipofika Ikulu Zanzibar kwa ajili ya Mazungumzo na Rais.[Picha na Ramadhan Othman, IKulu]


“Tangu kuundwa chini ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa miaka miwili iliyopita Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwelekeo wa uchumi na ustawi wa Zanzibar umekuwa mzuri ambapo mbali ya kuongezeka kiwango cha kukua kwa uchumi lakini imeweza kupunguza kiwango cha mfumuko wa bei kutoka asilimia 23 Septemba mwaka 2011 hadi asilimia 4.4 Novemba mwaka 2012” alisema Dk Shein.

Dk. Shein alifafanua kuwa kushuka kwa kiwango cha mfumuko wa bei kunatokana na kuwepo na chakula kingi hali ambayo ni matokeo ya kuongezeka kiwango cha uzalishaji chakula Zanzibar na uagizaji chakula toka nje ingawa changamoto sasa ni uwezo mdogo wa wananchi wengi kununua chakula hicho.

“Serikali ya Serikali Umoja wa Kitaifa tuliiunda ili kuleta maelewano kati yetu kwa kudumisha amani na utulivu hivyo nimefurahi kuona katika kipindi cha miaka miwili tangu kuundwa kwake tumeweza kuwatumikia vyema wananchi kwa faida na maslahi yao” alimueleza Waziri huyo na ujumbe wake.

Hata hivyo Rais wa Zanzibar alibainisha kuwa pamoja na mwelekeo huo mzuri Zanzibar inakabiliwa na changamoto kadhaa wa kadhaa katika sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu na afya lakini alieleza matumaini yake kuwa kwa kushirikina na washirika wa maendeleo ikiwemo nchi ya Oman changamoto hizo zitapatiwa ufumbuzi na kufikia malengo yaliyowekwa.

“changamoto ni nyingi lakini Serikali na wananchi wa Zanzibar wamejidhatiti kupambana nazo na kwa kuungwa mkono na washirika wake kama Oman matumaini ni makubwa kwao” alisema.

Akizungumzia juu ya uhusiano kati ya Tanzania na Oman Rais wa Zanzibar alieleza kufurahishwa kwake na uhusiano wa nchi hizo mbili na kueleza kuwa umejengwa katika misingi ya usawa, ustawi na maslahi ya Serikali na wananchi wa nchi hizo.

“Ni uhusiano wa kihistoria na kindugu kati yetu (Tanzania na Oman) na umejidhihirisha na mashirikiano ya karibu kati ya Serikali na watu wa nchi zetu” alisisitiza na kutaja ziara za mara kwa mara kati ya viongozi wa nchi hizo pamoja na kusainiwa hivi karibuni kwa makubaliano kati ya nchi hizo kuwa ni vielelezo vya uhusiano huo ulivyo wa dhati.

Kwa upande wake, katika mazungumzo hayo, Waziri anayesimamia masuala ya Mambo ya Nje wa Oman Bwana Yousuf bin Alawi bin Abdullah amesema ziara yake nchini Tanzania imelenga kuimarisha uhusiano kati ya nchi yake na Tanzania.

“nimekuja kuimarisha uhusiano mwema uliopo kati ya Oman na Tanzania kwa nia ya kufanya kazi pamoja kwa ajili ya maslahi na ustawi wa nchi na wananchi wa nchi mbili hizi” amesema Waziri Yousuf.

Bwana Yousuf alimueleza Rais kuwa wakati wa ziara yake nchini alipata nafasi kuzungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo katika nyanja ya siasa, utamaduni, biashara na ukwezaji na kueleza kuwa mazungumzo hayo yamelekezwa katika kuziweka karibu Serikali na wananchi wa Oman na Tanzania. Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Oman Balozi Ali Ahmed Saleh na Mkuu wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Yahya Simba.