Mwamuzi wa FIFA Aondolewa Kuchezesha Ligi Kuu Bara

KOMBE LA LIGI KUU YA VODACOM TANZANIA BARA

Na Mwandishi Wetu

MWAMUZI Msaidizi wa FIFA, Ferdinand Chacha ameondolewa kuchezesha mechi za VPL baada ya kupata alama za chini kwenye mechi kati ya African Lyon na Simba iliyochezwa mwezi uliopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Waamuzi wanaopata alama 6.5 au chini ya hapo kati ya 10 zinazohitajika pia wanaondolewa kwenye mechi za VPL na FDL.

Waamuzi wengine walioondolewa kwa kutomudu mechi walizochezesha za VPL ni Mathew Akrama (Yanga vs Simba), Ephrony Ndissa (Yanga vs Simba), Ronald Swai (Yanga vs Mtibwa Sugar). Walioondolewa kwa kupata alama za chini ni Alex Mahagi (Simba vs JKT Ruvu), Methusela Musebula (Toto Africans vs Coastal Union), Lingstone Lwiza (Toto Africans vs Coastal Union), Idd Mikongoti (Toto Africans vs Mtibwa Sugar) na Samson Kobe (Toto Africans vs Mtibwa Sugar).

Masoud Mkelemi aliyekuwa mwamuzi wa mezani katika mechi ya FDL kati ya Moro United na Villa Squad ameondolewa kwa kutofika kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi (Pre-match meeting) na alichelewa kwa dakika tano kufika uwanjani.

MAKAMISHNA VPL/FDL WASIMAMISHWA, WAONYWA

Baadhi ya makamishna wa VPL na FDL wameondolewa na wengine kusimamishwa kusimamia mechi za ligi hizo kutokana na upungufu kwenye ripoti zao au kutowasilisha kabisa ripoti hizo TFF baada ya mechi. Kamishna Mohamed Jumbe aliyesimamia mechi kati ya Mgambo Shooting na Simba ameondolewa kwenye orodha ya makamishna kutokana na ripoti yake kuwa na upungufu.

Makamishna wa mechi kati ya JKT Oljoro vs Yanga (Hakim Byemba), JKT Oljoro vs Kagera Sugar (Salum Kikwamba), Toto Africans vs African Lyon (Charles Komba), Coastal Union vs JKT Oljoro (Mohamed Nyange) wamesimamishwa hadi watakapowasilisha ripoti zao TFF.

Kwa upande wa FDL makamishna waliosimamishwa hadi watakapowasilisha ripoti zao TFF ni wa mechi kati ya Kurugenzi vs Polisi Iringa, Morani vs Mwadui, Polisi Mara vs Pamba, Polisi Mara vs Mwadui, Morani vs JKT Kanembwa na Pamba vs Polisi Dodoma.

Wengine ni Mwadui vs JKT Kanembwa, Polisi Tabora vs Morani, Polisi Dodoma vs Polisi Mara, Polisi Tabora vs Mwadui, Polisi Mara vs Morani, JKT Kanembwa vs Polisi Mara, Morani vs Rhino Rangers na Small Kids vs Mkamba Rangers.

Kamati ya Ligi imewakumbusha makamishna wote kuwa ni jukumu lao kuhakikisha ripoti zao zimefika TFF na kurekebisha upungufu wa jinsi ya kuripoti matukio yanayotokea uwanjani. Licha ya kutuma nakala kwa njia ya email, wanatakiwa pia kuwasilisha ripoti halisi (original) TFF.

MECHI YA SIMBA, MTIBWA YAINGIZA MIL 62/-

Mechi namba 121 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa juzi (Februari 24 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Mtibwa Sugar kuibuka ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba imeingiza sh. 239,686,000.

Watazamaji 10,669 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 14,577,252.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 9,467,694.92.

Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 9,491 na kuingiza sh. 47,455,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 105 na kuingiza sh. 2,100,000.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,412,162.26, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 4,447,297.36, Kamati ya Ligi sh. 4,447,297.36, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,223,648.68 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,729,504.53.

VUMBI LA VPL KUENDELEA JUMATANO

Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Februari 27 mwaka huu) kwa mechi tano zitakazochezwa katika viwanja tofauti. Vinara wa ligi hiyo Yanga wataikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa viingilio vya sh. 5,000 (viti vya bluu na kijani), sh. 8,000 (viti vya rangi ya chungwa), sh. 15,000 (VIP C na B) na sh. 20,000 (VIP A).

Mechi nyingine za ligi hiyo ni Coastal Union vs Ruvu Shooting (Mkwakwani, Tanga), Polisi Morogoro vs Mgambo Shooting (Jamhuri, Morogoro), JKT Ruvu vs Toto Africans (Azam Complex, Dar es Salaam) na Mtibwa Sugar vs Tanzania Prisons (Manungu, Morogoro).