Na Isaac Mwangi, EANA
TIMU ya watu 40 yenye kujumuisha wajumbe kutoka nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) isipokuwa Kenya wamepelekwa nchini humo kuwa waangalizi katika uchaguzi mkuu ujao wa nchi hiyo utakaofanyika Machi 4, mwaka huu.
Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi huo inaongozwa na Spika wa zamani wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Abdulrahman Kinana wa Tanzania. Jukumu hilo pia litaratibiwa na mbunge wa zamani wa EALA kutoka nchini Uganda, Lydiah Wanyoto.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi juzi, Katibu Mkuu wa EAC Dk. Richard Sezibera alisema wajumbe wa timu hiyo wametoka katika maeneo mbalimbali lakini wakiwa na lengo moja la kulikamilisha.
“Timu inajumuisha wajumbe toka EALA, Tume za Uchaguzi za Taifa, Tume za Kitaifa za Haki za Binadamu na wawakilishi wa vijana toka Tasisi ya Mabalozi wa Vijana wa EAC. Uteuzi pia uanzingatia uwiano wa jinsia na vijana.”
Waangalizi hao Katibu Mkuu alisema,watakuwa waangalia jinsi kampeni zinavyofanyika,uandikaji wa habari za uchaguzi na vyombo vya habari na sheria zinazotawala utendaji wake, kazi ya uongozi wa uchaguzi wenyewe na wadau husika katika kipengele hiki na utatuzi wa migogoro itakayotokea katika uchaguzi huo.
“Timu hiyo itakutana na kushauirina na wawakilishi wa wadau katika uchaguzi huo na vyama vya siasa pamoja na wagombea wao na pia wawakilishi wa vyama vya kiraia, waandishi habari na jumuiya za kimataifa,” alisema Dk. Sezibera.
Timu ya EAC kwa mujibu wa Dk Sezibera, itaungana pamoja na timu ya Soko la Pamoja toka Kusini mwa Afrika (Comesa) na Mamlaka ya Wadau wa Maendeleo (IGAD) katika uratibu wa shughuli za uangalizi wa uchaguzi.
Akizungumza katika mkutano huo Kinana alisema suala zima la uchaguzi huo ni la Wakenya na jukumu la timu yake ni kuangalia yatakayotokea na kuandika ripoti juu ya uchaguzi huo.