Rwanda yajiunga na muhula wa vyuo vikuu Afrika Mashariki

Bendera ya Rwanda

Na James Gashumba, EANA

KIGALI, (EANA) -RWANDA imefanya maamuzi ya kuoanisha muhula wake wa vyuo vikuu ili uendane na vyuo vikuu vingine vya nchi za Afrika Mashariki.

Uamuzi huo umefanywa na baraza la mawaziri la nchi hiyo na kupongezwa na wanafunzi kwa kuwa sasa wanaweza kusoma katika nchi nyingine za Afrika Mashariki bila kuwa na mashaka ya namna ya kupata fedha na kuzihamisha kwa muda muafaka.

Kutokana na maamuzi yaliyofanywa na baraza la mawaziri, kuanzia mwaka huu muhula wa masomo kwa vyuo vikuu vya Rwanda utaanza Septemba. Awali Vyuo vikuu vya Rwanda vilikuwa vinaanza muhula wake Januari na kumalizikia Oktoba.

Joseph Maniraguha, mwanafunzi wa Chuo Kikuu Kigali Independent aliafikiana na hatua hiyo na kusema itasaidia sana, lakini akaelezea mashaka yake kwamba kutakuwa na kasi kubwa ya kutaka kumaliza muhula uliopo ifikapo Agosti ili kuwa sambamba na utaratibu huo mpya.

Aliliambia Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) kwamba hatua hiyo imekuja wakati muafaka na huku ikionesha kwamba nchi hiyo sasa inaingia moja kwa moja katika ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Naye Josiane Karegeya, mwanafunzi wa Chuo cha Fedha na Masuala ya Benki (SFB) kijulikanacho kama, School of Finance and Banking, aliwashauri wanafunzi wenzake kukubaliana na kasi ambayo itatumika kwa taasisi mbalimbali kukamilisha mitaala yao mapema ili kuendana na mabadiliko hayo.

Wataalamu wa masuala ya elimu wanaona kuwa kitendo cha kuoanisha kalenda ya masomo katika vyuo vikuu unahitimisha ndoto ya muda mrefu ya kuwa na mfumo mmoja wa elimu kwa nchi za Afrika Mashariki, ukiwemo wa kubadilisha mtaala wa sasa ili kukidhi mahitaji ya ushirikiano.

Waziri wa elimu wa Rwanda, Pierre Damien Habumuremyi alisema kwamba kuoanisha kwa kalenda hiyo kutawawezesha wanafunzi kuweza kuhamisha fedha za masomo na kuendelea na masomo yao bila ya kuyavuruga.

Maamuzi hayo ya Rwanda yanafanyika wakati Mataifa ya Afrika Mashariki yapo katika mazingira ya kutaka kuoanisha mfumo wa elimu, jambo ambalo linafanyiwa utafiti kwa sasa.

Mkurugenzi wa Elimu ya Juu wa Rwanda, Profesa Geoffrey Rugege, amesema ni matumaini yake kuwa utaratibu huo mpya utasaidia kuondoa ucheleweshaji wa wanafunzi kujiunga na vyuo vikuu.

Wanafunzi wanaowania kuingia Chuo kikuu walikuwa na kipindi cha kusubiri cha mwaka mzima lakini kwa utaratibu huo mpya hawatasubiri kwa muda mrefu, alisema Rugege.

Alisema mfumo huo mpya una maslahi mengi kiutendaji hasa kwa kuwa unaanza kipindi cha mwaka wa fedha kikiwa tayari na pia unawezesha kuwapo na mpango mpya wa ufundishaji ambapo kila muhula unapoisha na unamalizika na maksi zake.

Tayari baadhi ya taasisi za elimu ya juu nchini hapa zimeshaandaa mpango wa kufuatia ili kwenda sawa na mabadiliko hayo.

Dk. Reid Whitlock, mkuu wa SFB, aliwaambia waandishi wa habari kuwa chuo chake kimerekebisha muhula wake kwa mwaka kutoka miezi kumi hadi minane. Kutokana na mabadiliko hayo muhula wa mwaka huu utamalizika Agosti na Septemba wataanza muhula mpya.