MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2012: WATOTO WA MASIKINI WAMEACHWA PEMBEZONI
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP), tumekuwa tukifuatilia kwa karibu masuala mbalimbali yanayoihusu jamii hapa nchini ikiwa ni sehemu ya kudai mabadiliko ya mfumo wa uchumi, sera sheria na bajeti ili kuhakikisha kuwa raslimali za Taifa zinatumika kwa manufaa ya wananchi wote wanawake na wanaume hususani wale waliotupwa pembezoni.
Suala la elimu bora ni la msingi ndio maana kwenye madai yetu ya elimu ni pamoja na upatikanaji wa elimu bora ambayo ni sanjari na vifaa, chakula, mabweni hasa ya wasichana, walimu wenye ujuzi na mazingira rafiki ya kufundishia wanafunzi wote wa Kitanzania wanawake na wanaume.
Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne uliofanyika Oktoba 2012, yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa(NECTA) yametutia wasiwasi juu ya mustakhabali wa elimu nchini kutokana na kiwango cha ufaulu kwa wasichana kushuka kwa kasi kubwa ukilinganisha na mwaka jana. Kutokana na matokeo haya kunahitakija uwajibikaji wa dhati kwa watendaji wa Wizara ya Elimu na Baraza la Mitihani(NECTA).
TGNP tumesikitishwa sana na matokeo hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yanadhalilisha dhana ya Usawa wa Kijinsia katika mgawanyo wa rasilimali hasa katika sekta ya elimu imekufa. Tunasikitika kuwa taifa hili litakosa wataalam hasa wanawake wataalam kwa miaka ijayo.
Matokeo ya Jumla
Katika matokeo haya ya mwaka 2012 Jumla ya watahiniwa wa shule 126,847 kati ya watahiniwa 397,136 waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2012 wamefaulu. Wasichana waliofaulu ni 46,161sawa na asilimia 48.36, Hali inazidi kuwa mbaya ukilinganisha na mwaka 2011, wasichana waliofaulu walikuwa 74,667 sawa na asilimia 51.64% . Tunaona kuwa wasichana waliofaulu ni nusu ya wavulana waliofaulu, je hapo kuna usawa wa kijinsia? Je hali ikiendelea hivi tutapata kina mama wasomi miaka 20 ijayo?
Ubora wa ufaulu kwa madaraja na Jinsia
Ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule unaonesha kuwa jumla ya watahiniwa 23,520 wamefaulu katika madaraja I – III ambapo kati yao wasichana ni 7,178 na wavulana ni 16,342. Ambapo pia wasichana ni chini ya asilimia 50 ya waliofaulu. Tunaandaa taifa lenye wasomi wa aina gani kama wanawake hawataweza kifika Chuo Kikuu?
Tumestushwa na kauli hii ya serikali kukiri udhaifu wake ambao kila mara sisi wanaharakati tumekuwa tukilalamika na kuhoji juu ya uboreshaji wa mazingira ya kazi ikiwepo, kupatikana kwa vifaa vya kutosha mashuleni. Tunajiuliza ni kwanini serikali haikuchukua hatua mapema licha ya kelele za wananchi kwa muda mrefu.
Kutokana na takwimu hizi inasikitisha kuona idadi kubwa ya wasichana watakao baki mitaani bila kuendelea na masomo ya juu. Pia kutokana matokeo hayo, wasichana wengi hawataweza kujiunga na vyuo vya elimu ya juu, wala ualimu kwa sababu wamepata madaraja ya chini yaani daraja la Nne na sifuri. Madhara yanayojitokeza hivi sasa ya wanafunzi kujinyonga ni dhahiri kuwa matokeo ni kinyume na maandalizi yao. Serikali na Baraza la Mitihani wanatakiwa kuwajibika kwa hili.
Tunasikitishwa kwa sababu bado serikali haijafanya kazi kubwa ya kuziwezesha shule zake ambazo kimsingi zimebakia kuwa shule za watoto wa masikini wasioweza kumudu gharama kubwa za elimu. Bado serikali haina mitaala ya kufundishia kama ilivyobainika katika mkutano wa 10 wa Bunge ulipita. Bila kuwa na mtaala wa kudumu na unaoeleweka hali itaendelea kuwa mbaya. Kutokana na utafiti wa kiraghibishi uliofanywa na TGNP Mbeya Vijijini, Kishapu na Morogoro mwanzoni mwa mwaka jana ulionekana wazi kwamba maeneo mengi hasa ya vijijini wanafunzi wengi hasa wasichana hawana makazi rafiki na salama yaani mabweni, vifaa vya kusomea, walimu na maji. Kutokana na hilo, tunaitaka serikali kufanya yafuatayo:-
• Waziri Dk. Shukuru Kawambwa na watendaji waandamizi wa Wizara wajiuzulu kutokana na udhaifu wa wizara yao kwa kipindi kirefu.
• Kusimamisha ujenzi wa shule mpya za sekondari na kuanza mkakati endelevu wa kuziimarisha zilizopo na kuzipatia vitendea kazi vya kutosha kama mabweni,vitabu,walimu, maabara, maji safi, chakula cha mchana na vifaa vya kufunidishia.
• Maslahi ya walimu wa shule za kata na nyingine yaboreshwe, waalim walipwe malimbikizo ya mishahara yao, wapatiwe vitendea kazi, na nyumba za kuishi zenye maji na umeme au umeme wa jua kwa vijijini.
• Huduma za kijamii kama vile masoko, chakula na afya ziboreshwe vijijjini ili kuwapa walimu moyo wa kufanya kazi.
• Serikali ihakikishe kila shule ya kata inapata walimu wa masomo yote pamoja na sayansi.
• Tunaitaka serikali kuandaa mitaala ya elimu na kuisambaza mashuleni ili kuimarisha na kuboresha elimu ya Tanzania.
• NECTA iangalie upya mfumo wa usahihishaji wa mitihani kama kuna kasoro zitakazobainika matokeo yote yaliyotangazwa yabatilishwe kabla ya kuleta madhara zaidi.
TGNP tunaitaka serikali ibadilishe sera ya elimu ya sekondari iliyopo kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wa sekondari wasichana na wavulana wa tajiri na masikini, wa vijijini na mijini wanapata elimu sawa,bora na yenye haki.
Imetolewa na:
Lilian Liundi
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji TGNP