MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal atakuwa Mgeni Rasmi katika sherehe za ufunguzi wa barabara ya Kilwa (Sehemu ya Mtoni Mtongani hadi Mbagala Rangi Tatu) iliyoko jijini Dar es Salaam. Sherehe hizi zimepangwa kufanyika siku ya Jumamosi ya tarehe 23 Februari 2013 katika viwanja vya Zakhem; Mbagala.
Sehemu itakayofunguliwa inakamilisha awamu tatu zilizojengwa katika barabara ya Kilwa kama ifuatavyo:-
· Bendera Tatu hadi Mtoni Mtongani yenye urefu wa kilometa 5,
· Mtoni Mtongani hadi Mbagala Rangi Tatu yenye kilometa 5.1, na
· Mbagala Rangi Tatu kuishia Mbagala Zakhem yenye urefu wa kilometa 1.5.
Sehemu ya Mtoni Mtongani hadi Mbagala Rangi Tatu ililazimika kurudiwa na Mkandarasi M/S Kajima kwa gharama zake kutokana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuikataa baada ya kubainika kuwa ilikuwa imejengwa chini ya viwango. Marudio ya ujenzi huo kwa sasa yamekamilika na iko tayari kwa ufunguzi huu ambao utafanywa na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal.
Kukamilika kwa mradi huu kumepunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa magari uliokuwepo hapo awali ikizingatiwa kwamba barabara hii ni kiungo cha kutokea Bandarini kuungana na barabara nyingine zinazotoka nje ya jiji la Dar es Salaam. Aidha, barabara hii inahudumia viwanda vingi na viwanja vikubwa vya michezo na maonyesho katika wilaya ya Temeke. Vile vile Barabara ya Kilwa inauunganisha mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara. Hivyo Barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi kwa jumla.
Taarifa hii imetolewa na; Balozi Herbert E. Mrango
KATIBU MKUU