MWANARIADHA mlemavu wa Afrika Kusini Oscar Pistorius alimuua mpenzi wake kimakosa baada ya kudhania kuwa alikuwa mwizi aliyekuwa amevamia nyumba yake. Aliiambia mahakama kuwa alimpenda mchumba wake Reeva Steenkamp na wala hakuwa na nia yoyote ya kumuua kama ilivyotokea. Viongozi wa mashtaka wanamtuhumu Pistoriusa kwa mauaji wakisema alikuwa amepnga kumuua mchumba wake baada ya kumpiga risasi mara tatu na kumuua akiwa ndani ya bafu nyumbani kwake.
Taarifa kuhusu mauaji hayo zimeanza kujitokeza katika kesi ambapo jaji ataamua ikiwa atampa Pistorius dhamana au la. Haya yamejitokeza kwenye maelezo ya viongozi wa mashtaka huku mazishi ya mwanamitindo huyo yakifanyika mjini Port Elizabeth.
Viongozi wa mashtaka wanasema kuwa Oscar alimuua Reeva baada ya kupanga mauaji yake. Madai anayotarajiwa kuyapinga vikali. Pistorius alibubujikwa na machozi alipokuwa anasikiliza maelezo ya viongozi wa mashtaka, lakini mawakili wake walisema kuwa mauaji hayo hayakupangwa.
Mchumba wake aliyekuwa mwanamitindo, Reeva Steenkamp, aliuawa siku ya Alhamisi. Polisi waliweza kupata bunduki katika eneo la mauaji. Bwana Pistorius aliwasili mahakamani kabla ya saa tatu asubuhi ambayo itakuwa mara ya kwenzi kesi hiyo inasikilizwa tangu alipozuiliwa na polisi na kulia mbele ya mahakama Ijumaa wiki jana.
Viongozi wa mashtaka wanatarajiwa kuwasilisha ushahidi wao dhidi ya Pistorius wakisema anyimwe dhamana kabbla ya kesi yake kuanza kusikilizwa. Pistorius pia huenda akajitetea kwa mara ya kwanza tangu kesi yake kuwasilishwa mahakamani.
Mwanariadha huyo asiye na miguu yote alishikwa na polisi mwishoni mwa wiki na hajazungumza hadharani tangu mauaji hayo kufanyika. Taarifa kutoka kwa familia ya Pistorius ilisema kuwa atakanusha madai yote yanayoandaliwa dhidi yake.
Wakati huohuo, familia ya marehemu imeelezea masikitiko yao kwenye jarida moja iliyochapishwa siku ya Jumatatu. Mamake Marehemu alisema kile wanachotaka ni majibu tu, majibu ya kwa nini mauaji hayo yalifanyika kwa nini mwanao alifariki kwa njia hii.
Kesi ya Oscar kutaka kuomba dhamana haitapeperushwa hewani baada ya mawakili kukataa. Aidha kesi inayomkabili Oscar imezua hisia kali nchini Afrika Kusini na kote duniani kwani mwanariadha huyo anasifika kama shujaa duniani kote. Anasifika kama mwanariadha mlemavu aliyeshindana na wanariadha wasio walemavu katika michezo ya olimpiki mjini London.
-BBC