Mlemavu wa miguu aomba msaada Songea

Pichani ni mlemavu huyo

Songea

UONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Matarawe Kata ya Matarawe eneo la Asia Kovu unatakiwa kujivua gamba, baada ya kushindwa kuwapa huduma ya utambulisho wa barua mlemavu mmoja aliyeahidiwa kupewa msaada na CCM makao Makuu.

Mlemavu wa miguu Adamu Mohamed aliomba msaada makao makuu ya CCM Dodoma, yakupewa msaada wa usafiri ama mtaji wa biashara kutokana na ulemavu wake.

Makao Makuu ya CCM yalikiri kupokea barua yake na kumpa matumaini kwa barua CCM/U. GO/34/403 ya tarehe 03/04/2009 barua ambayo ilitaka ngazi ya Tawi Kata yake ijue tatizo lake ili makao makuu yajue namna ya kumsaidia.

Tokea tarehe ya barua hiyo hadi leo Adamu Mohamed anapigwa danadana kana kwamba ni mtu mwenye viungo timamu, hakuna kiongozi wa Tawi wala Kata anayempa jibu linalotoa majibu ya barua iliyotoka Ccm makao makuu Dodoma.

Alipoulizwa kama Tawi lake la Matarawe lingeweza kumpa msaada wa usafiri ama mtaji anaohitaji alisema viongozi wote niliokutana nao wanasema hawana uwezo na Tawi halina uwezo wa kutoa msaada; “Je, mbona wanashindwa kunipa barua kuarifu Ccm Dodoma juu ya maamuzi yao ili makao makuu yaniokoe na hali yangu,” alisisitiza Mohamed.

Mohamedi ni mfanyabiashara ya kuuza mkaa eneo la Soko la Matarawe katika Manispaa ya Songea, mkaa ambao analetewa na tajiri yake ajulikanaye kwa jina maarufu la MASAI.

Matukio ya kutia moyo kwa mlemavu huyo ni kwamba katika baiskeli yake mbovu anayetembelea wakati huu ina bendera sita, Moja ya Hayati baba wa Taifa Mwl. J. K. Nyerere mbili za Rais aliye madarakani Jakaya Mrisho Kikwete bendera mbili za chama cha Mapinduzi na bendera nyingine ya Muungano wa Tanzania, Hii ni ishara tosha ana uzalendo na nchi yake.

Naye mzee mmoja Kiongozi wa Tawi la CCM Matarawe amabaye hakutaka jina lake litajwe amesema Tawi la Matarawe sasa lina tatizo la Uongozi kwani Mwenyekiti hayupo na baadhi ya viongozi hawapo Madarakani, uongozi huo unatakiwa kusukwa upya.

Hata hivyo alisifu juhudi za Adam Mohamed katika Kampeni mbalimbali na amesema hata watu wengi wanamkashifu vile anavyojituma kupiga debe kwa uzalendo alionao kweli ana stahili kusaidiwa “mlemavu kama huyo Adam ana washinda hata watu wazima kwa uzalendo “amemalizia mzee huyo, Aameshauri Kata ya Matarawe wampe barua ya utambulisho CCM Dodoma ili apate msaada anaohitaji.
CHANZO; Jambo Leo.